Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Mhe. Selemani Jafo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Gairo kwa kutekeleza maagizo ya serikali kwa maendeleo mazuri ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya halmashauri.
Mhe.Jafo Ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la jengo hilo la kisasa ambapo ujenzi wake unakaribia asilimia 75.
Akizungumza katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Gairo,
Mhe.Jafo alisema halmashauri hiyo imekuwa ya mfano kwa kutekeleza maagizo ya Serikali.
Pia aliwapongeza halmashauri kwakuamua kujichimbia kwenye ujenzi kwa kutumia mkandarasi Pacha Construction Company ambaye amefanya kazi kubwa na nzuri ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo, Naibu Waziri Jafo amewaagiza makatibu Tawala wa mikoa yote ambayo halmashauri zao zilipatiwa fedha lakini bado hawajaanza ujenzi mpaka sasa wawasilishe majina ya halmashauri hizo kabla ya Oktoba 10, mwaka huu ili mchakato wa kuzihamisha fedha hizo ufanyike mara moja kwa kuzipeleka fedha hizo katika halmashauri zinazo endelea na ujenzi kwasasa.
Katika hatua nyingine, Jafo amekagua ujenzi wa barabara za Gairo mjini huku akimhimiza meneja wa wakala wa barabara vijijini(Tarura) kuhakikisha anasimamia ujenzi huo ili ifikapo mwaka 2019 ahadi zote alizozitoa Rais Dk.John Magufuli katika barabara za halmashauri hiyo ziwe zimekamilika.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.5 inajengwa na mkandarasi C.G.I contractors LTD.
Akikagua barabara hiyo amewahakikishia wananchi kuwa serikali itafanya jitihada katika kuhakikisha barabara zinajengwa na kwa kiwango kinachotakiwa na kutoa fedha kwa wakati ili mkandarasi aliyepo aweze kumaliza kazi kama ilivyopangwa. Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo mkandarasi Stephen Aloyce amesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 70 na kuiomba serikali kukamilisha malipo ya shilingi Bilioni 1.5 ili kumalizia kazi iliyobaki kabla ya kipindi cha mvua kuanza.
Naye, Mbunge wa jimbo la Gairo Ahmed Shabiby ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi huku akiiomba serikali kuwasaidia kutatua kero ya maji ambayo bado inawaumiza wananchi wa Halmashauri ya Gairo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 715240010
Simu ya Kiganjani: +255 715240010
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa