Na. Cosmas M. Njingo. MOROGORO
Agosti 3.2023
Serikali imeendelea kuweka mpango mkakati kwenye sekta ya kilimo ambacho kitachangia 10% ya Pato la Taifa ifikapo 2030 hivyo kukuza uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa Agosti 1, 2023, mjini Morogoro na Mhe. Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro.
Mhe. Mizengo Pinda alisema Serikali inalenga kuwezesha Wakulima kulima kilimo chenye tija ambacho kitasaidia kuchangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa, na kuongeza kuwa Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo ambapo, lakini ni 15% ya ardhi hiyo ndiyo pekee inatumika kwa shughuli za kilimo na Mifugo.
“Mpango ambao tunakuja nao Serikali, tunataka tuone unaleta matunda ndani ya muda mfupi kadri itakavyowezekana lakini lengo kubwa mpaka ifikapo 2030 tuwe tumesukuma kilimo kiweze kuchangia angalau 10%...” amesema Mhe. Mizengo Pinda.
Katika hatua nyingine, Mhe. Pinda amesikitishwa na udumavu wa watoto chini ya miaka 5 ambapo mama anakuwa amekosa lishe bora kwa maandalizi ya mtoto kuwa na afya bora, hata hivyo ameweka bayana kuwa Mkoa wa Morogoro una tatizo la udumavu kwa 30.6% ambapo mwanzo ilikuwa 35% ikiongozwa na Iringa yenye 56.9%, wakati Mkoa huo ni Mkoa wa uzalishaji wa chakula cha kutosha katika maeneo mengi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mizengo Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kufikia bilioni 970 huku akitaka fedha nyingi zielekezwe katika Sekta ya kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu bora, mbolea na viwatilifu wakati 2022/2023 bajeti ilikuwa bilioni 751.1 na 2021/2022 ilikuwa bilioni 294.2, hivyo kadri miaka inavyozidi kwenda na kasi inaongezeka Zaidi.
Kwa upande wake, Mhe. Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema miundombinu kama barabara katika Mkoa huo ni jambo la lazima kwani Mkoa huo umejipanga kuzalisha mazao ya kibiashara ikiwemo mpunga, wakati mkoa huo unauwezo wa kuzalisha tani milioni 2 za zao hilo, hivyo miundombinu ni suala muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Naye, Mhe. Abubakar Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Maonesho ya Nanenane kanda ya mashariki amesema kanda hiyo imejipanga kufanya vizuri katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji kwani kanda hiyo ni kinara wa viwanda vikiwemo viwanda vya sukari na kuwataka wananchi kushirikiana vema na wataalamu ili kulima kilimo chenye tija zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa