NA. COSMAS MATHIAS NJINGO. GAIRO
APRILI 25. 2024
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava amewaagiza Afisa Maliasili na Misitu kupitia Kitengo cha Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, pamoja na Wakala wa Huduma na Uhifadhi wa Misitu (TFS) kuendelea kutoa Elimu Kwa Wananchi Wilayani humo kuhusu utunzaji wa Mazingira na kupanda miti kwa wingi.
Ametoa wito huo Aprili 21.2024 wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru zilipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo Mradi wa Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ng'holingo Kata ya Madege kwa ajili ya kuona ukamilishaji wa Ujenzi wa Zahanati hiyo ilijengwa kwa nguvu za Wananchi na mchango wa Serikali kwa ajili ya umaliziaji
”Nendeni kwa Wananchi mkawaelimishe umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira. Lakini pia Serikali imeelekeza kila Halmashauri ihakikishe miti 1,500,000 (milioni Moja na laki Tano) inapandwa kwa mwaka”. Alisema Kiongozi huyo.
Mnzava alisema Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge 2024 inasisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira na Jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi wa viongozi Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba 2024. Na kwamba viongozi waapaswa kuweka msisitizo mkubwa kwa Jamii kupanda miti na kushiriki uchaguzi huo.
Miradi mingine iliyofikiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 ni Mradi wa Upanuzi wa Huduma za Maji Iyogwe-Kinyorisi katika Kijiji cha Iyogwe Kata ya Iyogwe, Mradi wa Sekta Binafsi wa Ujenzi wa Nyumba ya Kulala Wageni J5, Mradi wa Ujenzi wa Vyumba 3 vya madarasa na matundu 3 ya vyoo Shule ya Msingi Lukungu iliyopo Kata ya Ukwamani.
Aidha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 pia zilizopita na kuona Mradi wa Kitalu Cha Miche ya Miti ya Parachichi ipatayo 15,000 unaosimamiwa na Halmashauri pamoja na kuweka jiwe la Msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Nyumba 3 za Wakuu wa Divisheni kitongoji cha Malimbika Kata ya Gairo
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge 2024 ni "Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu"
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa