Gairo – Mei 21, 2025
Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Gairo limeidhinisha rasmi mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, katika kikao maalum cha kupitia na kutathmini utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 na kutoa mapendekezo kwa bajeti ijayo.
Kikao hicho muhimu kimefanyika katika ukumbi mkuu wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na kuhudhuriwa na watumishi kutoka idara na vitengo mbalimbali pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu wa Baraza hilo alieleza kuwa kupitia tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita, mafanikio kadhaa yalipatikana ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, kilimo na miundombinu. Hata hivyo, alibainisha pia changamoto zilizoathiri baadhi ya maeneo ya utekelezaji, ikiwemo ucheleweshaji wa fedha kutoka Serikali Kuu na upungufu wa watumishi.
Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, aliipongeza timu ya wataalamu na watendaji wote kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uandaaji wa bajeti mpya, akisisitiza kuwa bajeti ya 2025/2026 imelenga kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi, kukuza uchumi wa ndani na kuongeza uwajibikaji kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi.
“Baraza hili limekuwa jukwaa muhimu la maamuzi ambapo watumishi wanashiriki moja kwa moja katika kupanga vipaumbele vya maendeleo ya Halmashauri. Tunatarajia utekelezaji wa bajeti ya mwaka ujao utaendana na matarajio ya wananchi wetu,” alisema Mkurugenzi.
Wajumbe wa Baraza hilo walitoa mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha bajeti hususan katika maeneo ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma, pamoja na kushirikisha jamii katika miradi ya maendeleo.
Kwa pamoja, Baraza lilikubaliana na mpango uliowasilishwa na kuuridhia kwa hatua zaidi za uwasilishaji kwa mamlaka za juu kwa ajili ya kupitishwa rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa