Naibu Waziri Wa Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Dakta Festo John Dugange amewagiza Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi yote na kwamba miradi hiyo inatakiwa kukamilika kwa muda uliopangwa ili ianze kutoa huduma zilizokusudiwa katika kuwaletea maendeleo Wananchi.
Ametoa agizo hilo Juni 20, 2021 katika kikao cha ndani na Viongozi wa Wilaya, Watendaji wa Halmashauri pamoja na watumishi wa Idara ya Afya wakati wa ziara yake kukagua hali ya utekelezaji wa ujenzi wa majengo saba ya Hospitali ya Wilaya ya Gairo pamoja na ujenzi wa boma kwenye zahanati ya Mogohigwa iliyopo kata ya Chigela.
“Nakuagiza Mkurugenzi ukishirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri, hebu kasimamieni kwa ukaribu miradi yote na mhakikishe inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma tulizo kusudia hususani kwa hii miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na zahanati mpya ya Mogohigwa, lakini pia hata kwa miradi ya urekebishaji miundo mbinu kwenye zahanati za zamani”, alisema Dakta Dugange
Alifafanua kuwa ni lazima pawepo na usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya kupitia miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya, uboreshaji wa miundominu kwenye kituo cha afya na zahanati pamoja na ujenzi wa zahanati mpya ili thamani ya pesa ilingane na ubora wa majengo yaliyopo na miundo mbinu mingine.
"Mkurugenzi hili nalo ni muhimu sana kulizingatia, Serikali inaleta fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya afya, lengo ni kuhakikisha Wananchi wake wananufaika na ubora wa huduma, hivyo thamani na ubora wa majengo pamoja na miundo mbinu yake lazima ilingane kabisa na thamani ya fedha zilizotumika”, alisisitiza.
Kwa upande mwingine alipongeza kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kuemsa kuwa juhudi za Halmashauri zinaonekana ingawa alibaini kasoro ndogo ndogo zilizo jitekeza ambapo alitoa maelekezo kasoro hizo zirekebishwe haraka kwa kipindi cha mwezi mmoja ili huduma zianze kutolewa hususani jengo la maabara ifikapo Julai 20, 201.
Alidai “Umaliziaji siyo mzuri sana, nadhani kulikuwa na shida katika usimamizi kwa mafundi mliowapa kazi hii. Hapa jicho langu lipo kwa Mkurugenzi kama msimamizi Mkuu, Mgangan Mkuu Wilaya na Mhandisi wa ujenzi mmeonyesha udhaifu, ingawa ninawapongeza kwa kasi nzuri ya ujenzi na majengo ni mazuri lakini umaliziaji wake kidogo bado sijaridhishwa nao”.
Aidha kwa upande mwingine Dakta Dugange amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri Bi Agnes Mkandya pamoja na Mweka Hazina Wilaya kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhakikisha wanafikia lengo la 100% ifikapo juni 30, 2021 kabla yam waka mpya fedha 2021/2022 kuaza.
“Swala la makusanyo kwa Gairo bado mpo chini sana ni 67% tu ya lengo, naagiza pia lipewe uzito zaidi ili kufikia Juni 30, mfike lengo la 100%. Kupitia makusanyo ya ndani mtakuwa na nguvu ya kujiendesha bila kuwa na utegemezi kutoka Serikali kuu, pia itasaidia kuimarisha miundombinu katika utoaji hudumwa kwa jamii’. Alisisitiza Naibu Waziri.
Hata hivyo Dakta Dugange alisisitiza swala la utawala bora, ushirikiano na ushirikishwaji kwa Viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya hadi kushuka chini kwenye vivjiji ili kuongeza kasi ya maendeleo badala ya kila mmoja kuzungumza lugha yake hali ambayo alisema inachafua sifa na hadhi ya Wilaya..
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa