Na. Cosmas Mathias Njingo
GAIRO, Aprili 26
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imepokea shehena ya mahitaji mbalimbali ya Vifaa Tiba na Dawa kutoka #BOHARI KUU YA BIDHAA ZA AFYA (MSD) kwa ajili ya Huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya.
Shehena hiyo ya Vifaa Tiba vilivyopokelewa Hospitalini hapo ni pamoja na Vitanda 100, Magodoro 120, Shuka 700 na Dawa za kutibu magonjwa mbalimbali.
Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Njile Mahela ameishukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayaongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Sekta ya Afya Wilayani humo hususani kwa kutenga fedha nyingi za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kupeleka vifaa tiba na dawa
"Ninaipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mhe.Dkt Samia, Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwekeza fedha nyingi za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo, pamoja na hii shehena ya Vifaa tiba na Dawa ambayo tumeipokea". Alisema Mganga Mkuu huyo.
Mahela akabainisha kuwa shehena hiyo ya Vifaa Tiba na Dawa, itasaidia kuongeza wigo na kuboresha utoaji wa huduma za Afya Hospitalini hapo kwa kuwa tayari baadhi ya huduma zilishaanza kutolewa.
Akaongeza kuwa pamoja na Serikali kupeleka vifaa Tiba na Dawa Hospitalini hapo, Halmashauri pia ilipokea Wataalam mbalimbali wa afya na Tiba ikiwepo madaktari Bingwa kupitia ajira ya mwaka 2022, na kwamba kwa mwaka huu Serikali inatarajia kuajiri watumishi wengine wa Divisheni ya Afya ambao watapangiwa katika Hospitali ya Wilaya kwa lengo la kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za Afya na kwa wakati sahihi.
"Kwa sasa Halmashauri yetu tutatembea kifua mbele kwani tunauhakika wakuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja, Dawa zipo za kutosha, Vifaa Tiba tumepata lakini pia tunao wataalam wa uhakika na watakao kidhi mahitaji ndani ya Wilaya yetu na wateja kutoka nje ya Wilaya". Alitamba.
Kwa upande mwingine, Dkt Mahela amewataka wakazi wa Gairo na Wilaya jirani kufika hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za afya, ili kupunguza msongamano katika kituo cha afya ambacho kwa miaka mingi kimekuwa kikitoa huduma kama hospitali ya Wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa