Cosmas Mathias Njingo;
Gairo, MOROGORO.
Disemba 2.2022.
Katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na UKIMWI, huduma zimeendelea kuboreshwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwawezesha Watu wanaoishi na Virusi hivyo (WAVIU) kupata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao.
Hayo yamebainishwa kwenye risala iliyosomwa mbele ya Mgeni Rasmi Mheshimiwa Jabiri Omari Makame, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, na mmoja wa WAVIU katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani, ambayo kiwilaya yaliazimishwa katika kijiji cha Leshata kata ya Leshata Disemba 1.2022.
“Katika kupambana na V.V.U na UKIMWI, utoaji wa huduma kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI imeboreshwa hasa kwenye vituoa vya ushauri nasaha, Upimaji wa V.V.U, upimaji wa CD4 na utoaji wa Dawa za kufifisha makali ya V.V.U; pamoja na kuongeza vituo vya kutolea huduma hizo”. Ilisema sehemu ya Risala hiyo.
Kwa mujibu wa Risala hiyo kwa Mgeni Rasmi, hapo awali WAVIU walikuwa wakikabiliwa na upungudu wa vituo vya kutolea huduma, ambapo kulikuwa na kituo kimoja tu, ambacho ni Kituo cha Afya Gairo. Hali ambayao iliwalazimu kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hizo na kuwasababishia usumbufu mkubwa.
“Uboreshaji wa huduma kwa WAVIU ni pamoja na kuongeza vituo vya kutolea ushauri nasaha, vipimo na ugawaji wa dawa za ARV (CTC), kutoka kituo kimoja hadi vituo sita. Hii imetupunguzia kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo, mfano wengine tulikuwa tunatoka kata za mbali kwenda kituo cha Afya Gairo”. Ilisema Risala hiyo.
Vituo vitano vilivyo ongezeka kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha huduma kwa WAVIU ni pamoja na Zahanati za Rubeho, Msingisi, Kibedya, Chakwale na Zahanati ya Chogoali, na kwamba uwepo wa vituo hivyo umerahisisha upatikana wa huduma kwa WAVIU waishio katika kata hizo na kata za jirani.
Kuhusu hali ya unyanyapaa, risala hiyo ilibainisha kwamba vitendo vya unyanyapaa kwa WAVIU bado vinaendelea licha ya elimu kutolewa kwa umma ya kupinga vitendo vinavyoashirikia unyanyapaaji; lakini vitendo hivyo vinajitokeza kwa baadhi ya jamii kuwanyanyapaa Watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, na upande mwingine WAVIU wamekuwa na tabia ya kujinyanyapaa wao wenyewe.
Risala hiyo imeeleza kuwa kutokana na vitendo vya unyanyapaa kuongezeka, waathirkika wengi wameshindwa kujitangaza kuhusu afya zao; na kwamba hali hiyo inachangia WAVIU wengi kuishi na msomgo wa mawazo na kusababisha kupoteza maisha mapema.
Aisha katika Risala yao WAVIU hao wameishauri Jamii na Wadau wote kwa ujumla kujitokeza kupima Afya zao kwa hiari, sambamba na kuimba Serikali kusaidia upatikana wa usafiri ili kuuwezesha uongozi wa KONGA kutekeleza majukumu yao ya kutoa elimu kwa umma juu ya kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.
Siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka, ambapo kwa Mwaka huu kilele cha Maadhimisho hayo Kitaifa kimefanyika Mkoani Lindi, na Mgeni Rasmi akiwa ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa