Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro imepokea gari lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 92,346,913.16 kwa ajili ya uboreshaji na kuimarisha ukaguzi, ufuatiliaji, usimamizi wa shughuli mbalimbali za Idara ya Elimu Msingi pamoja na utekelezaji wa miradi ya Elimu.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Afisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bwana Cosmas Njingo, Afisa Elimu Msingi Bwana Zakayo Mlenduka alisema Gairo ni Miongoni mwa Halmashauri 184 Tanzania Bara zilizo pewa magari hayo kutoka Serikali Kuu kwa kushirkiana na Mradi wa EP4R.
“Magari haya yalitolewa Mwezi Mei 2021 na Mhe. Kasimu Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ikishirikiana na Mradi wa EP4R ambao ni wadau wakubwa kwa Elimu nchini wamesaidia jumla ya Halmashauri 184 tanzania Bara”, alisema Bwana Mlenduka.
Afisa Elimu Msingi Bwana Mlenduka libainisha kuwa Gari hilo limekuja wakati muafaka kwani kwa kipindi kirefu sana Idara ya Elimu Msingi ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya usafiri wa uhakika hali ambayo alisema ilikwamisha kutekeleza majukumu ya idara yake na kwamba changamoto hiyo imepata ufumbuzi.
Alisema “Kwa kweli tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hasssan, Rais wa Jamhuri yauungano wa Tanzania kwa kutuongezea nguvu kwani kwa kupata gari hili shughuli na huduma za idara zitaimarika sana pia itakuwa rahisi kwetu kutembelea shule zilizopo pembezoni mwa mji wa Gairo na kutatua kero mbalimbali za walimu kule kule mashuleni badla ya kusubiri walimu waje makao Makuu ya Halmashauri kuleta malalamiko yao:.
Aliongeza kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu ikiwepo ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na ofisi za walimu lakini miradi mingi ilikuwa ikitekelezwa chini ya kiwango kutokana na idara hiyo kushindwa kutemnbelea miradi hiyo kwa ajili ya kukagua, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wake.
“Kimsingi kwetu kupata Gari hili ni fursa kubwa sana ya kutuwezesha kufanya ufuatiliaji wa karibu, kusimamia na kukagua shughuli za ujenzi wa miradi yote inayotekelezwa na Idara ya elimu Msingi kwa kuwa miguu ya kutembea na kufika popote kwa muda mfupi tunayo baada ya Serikali kutuongezea nguvu kupitia gari hili”, alitanabaisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa