Na. Cosmas Njingo-GAIRO DC
Idara ya maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro imejipanga vyema kuanza utaratibu mpya wa kutambua na kusajili vikundi vya vijana waendesha pikipiki maarufu bodaboda kwenye kata zao kupitia Watendaji wa Kata ili kurahishisha zoezi la kutambua vikundi vinavyohitaji kupewa mkopo wa 4% unaotolewa kwa ajili ya vijana.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Mohamd Amri amesema hayo kwenye kikao cha waendesha boda boda Wilayani humo kilicho itishwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabiri Makame na ofanyika katika ukumbi wa Diana Julai 19.2021.
“Mhe. Mkuu wa Wilaya, idara ya maendeleo ya Jamii imejipanga kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata katika zoezi la utambuzi wa vijiwe vyote vya waendesha boda boda Wilaya nzima ili kujua idadi ya vijana katika kila kijiwe kwa ajili ya kupanga utaratibu mzuri wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vitakavyo kidhi vigezo”, alisema Ndugu Amri.
Alisema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa majuma mawili (siku 14) likienda sambamba na usajili wa idadi ya vijana ambapo kila kijiwe kitasajiliwa na kutambulika rasmi chini ya Halmashauri pia kupitia mfumo huo itakuwa rahisi kwa idara hiyo kuendesha mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali ili kuviwezesha vikundi hivyo kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Tunaimani siku 14 zinatosha kabisa kufanya utambuzi wa vikundi vyote, hii itatusaidia kujua kijiwe kipi kina idadi ya boda boda wanagapi lakini pia idara ya Maendeleo ya jamii itaweza kuwafikia kwa urahisi hasa kupitia programu ya mafunzo na elimu ya ujasiriamali kwa vijana “, alisisitiza.
Akafafanua zaidi kwamba yamekuwepo malalamiko mengi kuhusu ucheleweshaji wa utaratibu wa kutoa mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu ambapo alisema tatizo kubwa linatokana na ufinyu wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwani ndiyo hugawanywa kwenye mikopo ya makundi hayo.
“Kwanza utaratibu wa kuchakata mikopo kwa haya makundi unategemea sana vyanzo vya ndani vya Halmashauri, lakini pia vipo vikundi ambavyo tayari vilishapewa mikopo na vinaendelea kurejesha kulingana na makubaliano yaliyopo kwenye mikataba, vikimaliza marejesho ndio vikundi vingine vitapewa mkopo kwa kuzingatia maombi”, alisema.
Aidha alibainisha kuwa Halmashauri inaendelea kutekeleza malekezo ya Serikali ya kuhakikisha inayafikia makundi yote yanayo stahili kupewa mkopo wa 10% ambapo alisema 4% zinaelekezwa kwa wanawake na vijana huku 2% zikilekezwa kwa wenye ulemavu na kwamba zaidi ya shilingi milioni 30 zimshatolewa kwa vikundi mbalimbali ikiwepo kikundi cha Rubeho Transporters ambacho kilikopeswa pikipiki 10 zenye thamani ya shilingi milioni 23 na laki tano.
Awali baadhi ya waendesha boda boda hao walilalamika kwa Mkuu wa Wilaya kuwepo kwa urasimu katika utaratibu wa upatikanji wa mikopo kwenye ofisi za Halmashauri, huku wakieleza kwamba wametuma maombi yao kwa muda mrefu lakini kila wanapo fuatilia wanajibiwa warudi kesho.
Mmoja wa vijana hao alisema” Mheshimiwa kuna tatizo kubwa pale Halmashauri, idara ya maendeleo ya jamii wanatuzungusha tunapo fuatilia maswala ya mikopo tunaambiwa rudi kesho, njoo kesho, hii hali inakutatisha tamaa sana hadi tumeamua kuachana na hiyo biashara ya mikopo”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Makame alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bi. Agnes Mkandya kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii kuhakikisha vikundi vyote vya waendesha boda boda vinasajiliwa na kutambulika rasmi sambamba na kuviwezesha kujikwamua kiuchumi kwa kuharakisha upatikanaji wa mikopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa