Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deo Mwanyika (MB), ametoa wito kwa wakulima wa parachichi katika Vijiji vya Masenge, Kata ya Rubeho na Mkobwe, Kata ya Chagongwe, kuhakikisha wanapanda miti na kutunza mazingira. Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo waliokuwa wakijifunza fursa za uwekezaji na kilimo cha mazao ya kimkakati.
Mhe. Mwanyika amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo, hasa katika maeneo yanayojihusisha na kilimo cha parachichi na viazi mviringo. Amesema kuwa upandaji miti utasaidia kuhifadhi ardhi, kuboresha hali ya hewa, na kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Aidha, Kamati hiyo imeipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa jitihada wanazofanya katika kuwekeza kwenye sekta ya kilimo. Mhe. Mwanyika pia amewahakikishia wakulima wa parachichi na viazi mviringo uhakika wa soko la mazao hayo, akibainisha kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha masoko ya mazao ya kilimo.
Ziara hiyo imelenga kuongeza uelewa wa fursa za uwekezaji kwenye kilimo, huku viongozi wakihimiza ushirikiano kati ya wakulima na serikali ili kufanikisha maendeleo ya sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa