Gairo – Februari 15, 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Kilimo na Mifugo imeahidi kuihimiza Serikali kuharakisha ujenzi wa Barabara ya Gairo–Nongwe ili kuboresha mawasiliano ya barabara na kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo katika Kata za Nongwe, Chagongwe na Masenge.
Amesema hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deo Mwanyika (MB), kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, wakati wa ziara ya kujifunza fursa zilizopo katika tarafa ya Nongwe, Wilayani Gairo, wakati akihutubia Wakulima wa zao la Parachichi na Viazi Mviringo kijiji cha Mkobwe kata ya Chagongwe, Februari 15.2025.
Mhe. Mwanyika amesema kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa maeneo hayo ambao wanategemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato, na kuongeza kuwa hali duni ya miundombinu ya barabara inakwamisha juhudi za wakulima kufikisha mazao yao sokoni kwa wakati, hali inayosababisha hasara na kupunguza tija katika sekta ya kilimo.
“Tunaihimiza serikali kupitia mamlaka husika kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara hii unapewa kipaumbele cha haraka. Miundombinu bora ya barabara ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya viwanda vidogo na kati, hasa vinavyotegemea mazao ya kilimo kama malighafi,” alisema Mhe. Mwanyika.
Ziara hiyo ya Kamati inalenga kutathmini fursa na changamoto zilizopo katika sekta za viwanda, kilimo na mifugo ili kutoa mapendekezo ya kisera na kibajeti yatakayosaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya vijijini.
Wakazi wa tarafa ya Nongwe wameipongeza Kamati hiyo kwa kujionea hali halisi ya miundombinu ya barabara na kutoa wito kwa serikali kutekeleza kwa haraka ahadi hiyo ili kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa