Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabiri Omari Makame amelishukuru na kulipongeza Shirika la Viwango Nchini (TBS) kwa kuendesha mafunzo kwa wadau wa kilimo Wilayani humo juu ya udhibiti wa Sumukukuvu kwenye nafaka hasa mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake.
Makame ametoa pongezi hizo Disemba 2.2021 katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya Udhibiti wa Sumukuvu kwa Wadau mbalimbali wa Kilimo Wilayani Gairo yanayo endeshwa na TBS kwa kushirikiana na Mradi wa TANIPAC uliopo chini ya Wizara ya Kilimo, katika kumbi za Diana, Msufini Pub na Ukumbi wa mikutano Hosipitali ya Wilaya ya Gairo.
“Ninaishukuru TBS kupitia mradi wa TANIPAC chini ya Wizara ya Kilimo kwa kutoa kipaumbele cha kuendesha mafunzo haya muhimu kwa Wananchi wa Gairo kuhusu elimu ya usalama wa chakula hususani katika udhibiti wa Sumukuvu kwenye Mahindi, Karanga pamoja na bidhaa zake”, alishukuru Mhe. Makame.
Makame alisema kuwa Gairo ni miongoni mwa Wilaya 18 nchini zinazotajwa kuwa na tatizo kubwa la Sumukuvu hali ambayo alisema inatishia usalama wa chakula na kuhatarisha afya ya Watumiaji wa nafaka hasa mahindi na karanga.
Alisema “Chakula kisicho salama husababisha madhara ya kiafya na vifo kwa walaji pamoja na athari nyingine za kiuchumi, hivyo ni wajibu wetu sote kuzingatia mikakati ya kukabiliana na changamoto ya Sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote”.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Mradi wa kudhibiti Sumukuvu TBS-TANIPAC Ndugu Jabiri Saleh Abdi alisema changamoto ya sumukuvu ni kubwa kwani inasababisha madhara kwa walaji na kwamba husababisha udumavu kwa watoto wadogo.
“Sumukuvu husababisha madhara makubwa kiafya kwa binadamu na Wanyama ikiwepo magonjwa ya kansa na vifo kwa binadamu, lakini pia hata huleta udumavu kwa watoto wetu kushindwa kuwa na ustawi mzuri katika ukuaji. Nahii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na Wizara ya Kilimo”, alifafanua Ndugu Abdi.
Uchafuzi wa sumukuvu unatajwa kuenea zaidi katika Mikoa 10 na Wilaya 18 nchini Tanzania ikiwemo Wilaya ya Gairo, ambapo TBS kupitia mradi wa kudhibiti sumukuvu TANIPAC umeanza kutoa mafunzo kwa Wakulima, Wafanya biashara za mazao, wasindikaji wa bidhaa zinazotokana na mahindi na karanga sambamba na wasafirishaji wa mazao kwa lengo la kuhakikisha changamoto hiyo inadhibitiwa kikamilifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa