Na. Cosmas M. Njingo. GAIRO DC
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigella amepiga marufuku Walimu Wakuu wa shule za msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari Mkoani Morogoro kuwatoza wazazi michango sambamba na kuwafukuzaMashuleni Wanafunzi wanaoshindwa kulipa michango hiyo.
Amepiga marufuku hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili Mei 25 na 26 2022 ya kutembelea miradi mbalimbali na kujionea utekelezaji wa shughuliza za maendeleo Katika Tarafa ya Gairo Wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro.
"Ni marufu kuwachangisha wazazi michango ya aina yoyote wala kuwafukuza wanafunzi mashuleni kwa kushindwa kuchangia michango hiyo". Alisema Shigella.
Akafafanua kuwa michango yote ijadiliwe kwenye kamati za shule, vikao vya wazazi, na kuongeza kwamba wakishakubaliana kuhusu michango hiyo muhtasari wa kikao husika uwasilishwe kwa Mkuu wa Wilaya ili atoe kibali endapo ataona inafaa baada ya kushirikishana na Mkureugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhusu bajeti za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya elimu.
"Ni lazima kwanza kuwepo na mijadala ya maridhiano baina ya kamati za shule na wazazi kupitia vikao, mkisha kubaliana mihutasari iwasilishwe kwa Mkuu wa Wilaya naye akishirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri aone bajeti ya utekelezaji wa maendeleo ya elimu imekaaje kisha atatoa kibali endapo ataona kuna ulazima wa kuwepo kwa michango hiyo", alisisitza.
Alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuweka mazingira rafiki ya kufundisha na kujifunza pamoja na kutoa fedha nyingi za elimu bila malipo kwa ajili ya uendeshaji wa shule ili kuhakikisha wazazi wanapunguziwa mzigo wa michango isiyo na tija.
"Haiwezekani Serikali inaleta fedha nyingi za elimu bila malipo kwa ajili ya uendeshaji wa shule zetu, halafu bado mnawatwishwa Wazazi mzigo wa michango, swala hili halikubaliki na sitaki liendelee kujitokeza", alionya Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika ziara yake Mheshimiwa Shigella alikutana na Wananchi wa Tarafa ya Gairo na kufanya mikutano ya hadhara kwenye kata za Chakwale, Rubeho na Ukwamani ambapo wananchi walipewa fursa ya kutoa kero zao mbele ya Mkuu wa Mkoa.
Kwenye kata zote tano ambazo zilifikiwa na Mheshimiwa Shigella wakati wa ziara yake Wilayani Gairo, pamoja na changamoto nyingine zilizo ibuliwa na Wananchi Mbele ya Mkuu wa Mkoa, kero kubwa iyotajwa katika mikutano yote ya hadhara ni uwepo ma michango mingi mashuleni, ambapo baadhi wa Wazazi pamoja na Wanafunzi walisema kufuatia michango hiyo wanafunzi wanaoshindwa kutoa hufukuzwa shule.
Wananchi hao wakahoji uhalali wa michango huku wengine wakiomba ufafanuzi kuhusu elimu bure wakati bado watoto wao wanaendelea kunyanyasika mashuleni na kukosa kuhudhuria baadhi ya vipindi madarasani baada ya kurejeshwa majumbani na walimu kwa kushindwa kutimiza agizo la ulipaji wa michango hiyo.
Kufuatia malalamiko hayo ikamlazimi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Shigella kumtaka Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Wilaya Bi. Nivoneia Levery kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizo ibuliwa na Wananchi hao, ambapo kabla ya kutoa maelezo Mhe. Shigella akapiga marufuku hiyo.
Akitoa ufafanuzi Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Bi. Levery pia akimwakilisha Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa yeye hana taarifa kuhusu uwepo wa michango mashule na kwamba amepokea malalamiko hayo atafuatilia ili kuona namna ya kutatua kero hiyo.
Mheshimiwa Shigela aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Sekretarieti ya Mkoa, ambapo alipokelwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabiri Omari Makame, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ndugu Shabani Sajilo, Katibu wa CCM Wilaya Bi. Queen, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bi. Rahel Nyangasi, baadhi ya Waheshimiwa Madiwani, Wajumbe wa KUU Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi. Susan Nyanda pamoja na baadhi ya wakuu wa idara na vitengo.
Timu hiyo kwa pamoja walitembelea miradi mbalimbali katika kata tano za Tarafa ya Gairo ikiwepo mradi wa Maji kijiji cha Kilama na Ujenzi wa Kituo cha Afya kata ya Iyogwe, Ujenzi wa Shule ya Sekondari kwa fedha za SEQUIP kata ya Leshata, maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika kata ya Gairo pamoja na kukagua hali ya uchimbaji madini katika mgodi wa dhahabu wa Kitaita uliopo kijiji cha kitaita kata ya Leshata.
Aidha Mkuu wa Mkoa Mhe. Shigela alifanya mikutani ya hadhara na Wananchi kwenye kata za Iyogwe, Leshata, Chakwale, Rubeho na Ukwamani ambapo mbali na marufuku hiyo aliwataka watendaji wa Serikali kuendelea kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa shughuli za maendeleo ili kuleta matokeo chanya sambamba na kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa