Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Siriel Mchembe na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Agnes Mkandya wameeleza mikakati waliyojiwekea katika kutokomeza mimba za utotoni Wilayani humo.
Wametaja mikakati yao katika mahojiano maalumu na mwandishi wa kituo cha runinga cha Azam wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kiwilaya yaliadhimishwa Juni 16, 2021 katika kijiji cha Mnyunhe kata ya Kibedya.
Mhe. Mchembe aliiambia Azam TV kuwa Wilaya yake imedhamiria kutokomeza mimba za utotoni kwa kuwachukulia hatua kali wanaume wote watakao bainika kuwarubuni watoto wa kike pamoja na kufanya msako mkali kwa wazazi wanao maliza kesi za mimba vichochoroni kwa kupokea rushwa ya pesa au mifugo.
Alisema wazazi wanapaswa kushirikiana na walimu, viongozi wa serikali ya kitongoji, kijiji au kata ikiwezekana hadi ngazi ya Wilaya, pindi wanapo baini watoto wao wamepata mimba ili wawatafuta na kuwatia mikononi mwa sharia wanaume wote wanaohusika na jambo hilo badala ya kumalizana kienyeji na watuhumiwa huku watoto wao wakikatisha ndoto zao za kuendela na masomo.
“Wilaya tumejipanga vizuri, kuhakikisha tunafanya sensa kwa wanafunzi wetu wa shule zote za msingi na sekondari ili kwanza kubaini hali ya utoro ipoje mashuleni, pili tujue sababu za utoro kama mimba ni chanzo basi tufanye kampeni kabambe kuwasaka wahusika wa mimba hizo na tatu tuchukue hatua stahiki kwa mujibu wa sharia”, alifafanua
Alieza kuwa hali ya mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari inazidi kuongezeka kwa kasi ambapo hadi sasa imeripotiwa mimba za utotoni Zaidi ya 100 hali ambayo alisema inatishia usalama na usatwi wa mtoto wa kike.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bi. Agness Mkandya alisema yeye na wataalam wake wa Halmashauri wamajipanga kutoa elimu kwa wananchi kupitia wenyeviti wa vitongoji na vijiji, watendaji wa kata na waheshimiwa madiwani kuhusu kampeni ya vita dhidi ya mimba za utotoni pamoja na walimu wakuu na wakuu wa shule zote.
“tumedhamiria kupambana na mimba za utotoni kwa nguvu zote nikishirikiana na wataalum wangu kutoka idara zote za Halmashauri katika kuendesha kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni kupitia mpango kabambe wa elimu kwa umma kuanzia ngazi za vitongoji hadi kata” alifafanua Mkurugenzi Mkandya.
Aidha alisema Halmashauri kwa kushirikiana na Serikali Kuu na wadau wengine wa elimu wataendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike katika kila sekondari ya kata ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu hali ambayo alisema itasaidia kuondoa vishawishi njiani na kupunguza matukio ya mimba.
“Tutaendelea kushirikiana na wadu wengine wa elimu wa ndani na nje ya Gairo pamoja na Serikali kuu kusimamia na kutekeleza ujezi wa mabweni ya wasichana sambamba na kuweka miundo mbinu ya kuwawezesha watoto kupata huduma zote muhimu, tunaamini mkakati huu utasaidia sana kuondoa hili tatizo la mimba kwa watoto wetu”, alisema Bi. Mkandya.
Kaui mbiu ya maadhimishi ya siku ya mtoto wa Afrika wma huu ni " Tutekeleza Agenda ya mwaka 2040, kwa Afrika inayolinda Haki za Watoto".
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa