Na. Asila Twaha,Tanga
Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kutoa elimu kwa jamii na kuweka mikakati thabiti ili kudhibiti uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko Nchini.
Hayo yamesemwa na Dkt. James Kengia kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais –TAMISEMI, katika kikao kazi cha Tathmini ya Programu ya utoaji wa Elimu ya Afya na Ushirikishwaji wa Jamii katika Majanga mbalimbali ya magonjwa ya mlipuko kilichofanyika mkoani Tanga Desemba 14, 2022.
“Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti magonjwa ya milipuko Nchinim ikiwepo kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa Wananchi juu ya kujikinga na Magonjwa yatokanayo na milipuko; sambamba na kuhakikisha tahadhari zote muhimu zinachukuliwa”. Alisema Dakta Kengia.
Dakta Kengia amewataka wataalam wa afya kwa kushirikiana na Wadau wengine ikiwepo Viongozi wa Dini kuendelea kutoa elimu wa jamii ya tahadhali mbalimbali za kujikinga na magonjwa ya milipuko ukiwepo Ukonjwa wa UVIKO-19
"Nitoe rai kwa wataalam wa afya kwa ngazi ya jamii, kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi ili mwananchi aweze kujikinga na magonjwa hayo, katika Ugonjwa wa UVIKO-19 tulishirikiana sana na viongozi wa dini katika kutoa elimu ya tahadhari, tuendelee kushirikiana nao ili tuwe na uwelewa wa pamoja" amesema Dkt. Kengia
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha miundombinu kwenye vituo vyote vya kutolea huduma, kununua vifaa tiba pamoja na kuendelea kuajiri wataalam wa afya ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Afya kutoka Idara ya Kinga Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma; Wizara ya Afya. Bw. John Yuda amesema, Serikali inao wataalamu ambao wanafanya utafiti katika kutafuta kinga na tiba sahihi ya magonjwa ya mlipuko ili kudhibiti maambukizi katika jamii.
“Tunao Wataalam wa Afya wenye uzoefu katika tafiti mbalimbali za kinga na tiba za magonjwa ya milipuko, hawalali wapo kazini muda wote wakiendelea kutafiti kinga na tiba sahihi za magonjwa ya milipuko. Hawa ni watu muhimu sana kwani kupitia tafiti zao watatuletea majibu kamili na kutupatia muongozo namna ya kudhibiti maambukizi katika jamii”. Alisema Dakta Kengia.
Katika maelezo yake, Dakta Kangia; amewataka wananchi kuendelea kuwasikiliza wataalamu wa afya kwa kuchukua tahadhari na kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa tishio wa Ebola ambao uneripotiwa kuenea Nchi jirani ya Uganda.
Naye Mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Chipole Mpelembe amesema mafunzo hayo ya siku tatu yatasaidia kuongeza weledi na mbinu bora za kuongeza uwajibikaji katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha, Wizara ya Afya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Waratibu Afya Jamii kutoka mikoa 13 ya Tanzania Bara iliyopo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Ebola, Wadau wa Maendeleo na Watafiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa