Na. Cosmas Mathias Njingo
GAIRO, Morogoro
Januari 3.2023.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, lililodumu kwa zaidi ya miaka 7, ambalo lilitolewa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2015.
Ametoa tamko hilo Januari 3, 2023, Ikulu Jijini Dar Es salaam, alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Nchini vyenye usajili wa kudumu.
“Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara’, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka”. Alisema Mhe.Dkt Samia.
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa katika wimbi la kilio kutoka kwa wanasiasa na jamii za kimataifa kuhusu haki ya kufanya shughuli za siasa ikiwepo kupigwa marufuku kwa mikutano ya hadhara, ambayo ipo kisheria kwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.
Hata hivyo baada ya Rais Samia kuingia madarakani mwaka 2021, kufuatia kifo cha Dkt. Magufuli, alionyesha dhamira ya kuleta maridhiano kwa kuunda kikosi kazi cha kukusanya maoni ili kupata muafaka na kurejesha mahusiano mema baina ya Serikali na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa.
“Lakini ndugu zangu tuna wajibu, wajibu wetu serikali ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema’, twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka, tukafanyeni siasa za kujenga sio za kubomoa, si kurudi nyuma hapa tulipofika, ‘sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa”. Alisema.
Mbali na kuondolewa kwa katazo hilo la vyama vya Siasa kutofanya mikutano ya hadhara, Mhe. Dkt Samia amesema Serikali inadhamiria kuhuisha mchakato wa marekebisho ya katiba mpya, uliokwama kwa zaidi ya miaka 8, toka mwaka 2014.
“Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba, kwa jinsi tutakavokuja kuelewana huko mbele, wengine wanasema tuanze na Katiba ya Warionba, wengine tuanze na Katiba pendekezwa, lakini kuna mambo ya ulimwengu yamebadilika” alisema.
Dkt Samia alisema atandaa Kamati maalumu kwa ajili kutoa ushauri wa namna ya kushughulikia upatikanaji wa katiba, na kuongeza kuwa katiba hiyo nia Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa au matakwa ya Vyama vya Siasa.
“Wakati mnanikabidhi kuongoza Nchi hii, busara zilinituma, kwamba jinsi nilivyolipokea Taifa hili, kuna haja ya kufanya Taifa liwe kitu kimoja, wote tuzungumze lugha moja; Ili Taifa lilwe moja, lazima tuwe na maridhiano, nikasema kwanza tuwe na mazungumzo kwenye vyama vya siasa”. Alieleza Mhe. Dkt Samia.
Rais Dkt. Samia alisema Kikosi kazi kilichoundwa kilikusanya maoni kwenye maeneo 9, huku swala la kutaka kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa likijitokeza mara kwa mara, mchakato wa katiba mpya na marekebisho ya sheria mbalimbali na kwamba tayari michakato ya marekebisho ya sheria imeanza na Waziri mwenye dhamana husika ataleta taarifa ya muelekeo wake.
Wanasiasa, akiwemo kiongozi Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo akizungumza kuhusu uamuzi wa huo wa Rais kukwamua mchakato wa katiba na kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa alisema ‘ni hatua kubwa sie tuna furaha, amesimama kwenye maneno yake’.
Mbali na Makamu wa rais Phillip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mkutano huo wa Rais na vyama vya siasa uliofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam, ulihudhuriwa na Wenyeviti, makamu wenyeviti na makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu kutoka vyama vote 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu Tanzania.
Vyama hivyo ni UPDP, NRA, TADEA, TPL, CHADEMA, CUF, NCCR, UDP na UMD.
Vingine ni chama tawala CCM, DEMOKRASIA MAKINI, DP, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMMA na ACT- Wazelendo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa