Nongwe, Morogoro – Februari 15, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema kuwa mkoa umejipanga kwa dhati kuhakikisha Wilaya ya Nongwe inakuwa mzalishaji namba moja wa zao la parachichi mkoani humo, kufuatia hali ya hewa ya maeneo ya tarafa hiyo kuonyesha kuafiki ustawi wa zao hilo kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Kilimo na Biashara, wakati wa ziara yao ya kukagua shughuli za kilimo katika Tarafa ya Nongwe, Mhe. Malima alieleza kuwa tayari hatua za utekelezaji wa mpango huo zimeanza kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kupandwa kwa hekta 227 za parachichi katika maeneo mbalimbali ya tarafa hiyo.
“Mpaka sasa tumeshapanda hekta 227 za parachichi, na tunatarajia kugawa miche 120,000 kwa vikundi vya wakulima ili kuhamasisha kilimo cha kisasa na biashara katika maeneo haya,” alisema Mhe. Malima.
Alibainisha kuwa lengo kuu la mkakati huo ni kuwasaidia wananchi wa Nongwe na maeneo jirani kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo biashara, huku serikali ikitoa msukumo katika kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, pamoja na huduma za ugani kwa wakulima.
Sambamba na jitihada hizo, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Mkoa wa Morogoro pia unaendeleza kampeni ya kuhamasisha uzalishaji wa zao la viazi mviringo (mbatata), ambalo pia linaonyesha mafanikio makubwa katika tarafa hiyo kutokana na rutuba ya udongo na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo hicho.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge walipongeza juhudi za Mkoa wa Morogoro na kutoa wito kwa serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu, masoko na elimu ya kilimo bora ili kuhakikisha wakulima wanapata faida kubwa kutoka katika kilimo cha parachichi na viazi mbatata..
Ziara hiyo ya Kamati inalenga kuona hali halisi ya utekelezaji wa shughuli za kilimo na viwanda kwa lengo la kuandaa mapendekezo ya kisera yatakayochochea maendeleo ya sekta hizo nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa