Cosmas Mathias Njingo;
MOROGORO.
Nov 16.2022.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.
Akifungua mkutano wa 15 wa mwaka wa wadau wa sekta ya uchukuzi wenye lengo la kufanya tathmini kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini, Prof. Mbarawa amesema ushiriki wa sekta binafsi, Serikali na wadau wa maendeleo utaharakisha ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege na meli na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kuhuisha miundombinu ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.
“Serikali tumejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara mpya ya Kibaha-Chalinze-Morogoro kilomita 215 (express way), ambapo mkandarasi atajenga kwa fedha yake na watakaotumia barabara hiyo watalipia,” amesema Prof. Mbarawa.
Amebainisha kuwa Serikali inajipanga kubadilisha Sheria ya TAZARA na TRC ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika huduma ya usafiri wa reli kwa kununua mabehewa mapya na kuyasimamia ili yawe na manufaa kwa Taifa zima.
Aidha Mhe. Prof. Mbarawa alisema ni muhimu kwa Tanzania kuwa na miundombinu bora kwa haraka ili kumudu kuhudumia kikamilifu soko la ndani la nchi sita ambazo hutegemea huduma ya uchukuzi kutoka Tanzania, ambazo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Kingdom Mbangula akizungumzia ujenzi wa barabara mpya ya kulipia, amesema barabara hiyo itakuwa na njia nne, mbili kwenda Morogoro na Mbili kurudi Kibaha na magari hayatapishana ili kuepusha msongamano na ajali.
“TANROADS tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mradi huu unajengwa kwa ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati,” amefafanua Eng. Mbangula.
Naye Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuandaa mkutano huo wa tathmini wa kila mwaka ambao unaibua changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.
Amesisitiza kuwa AfDB imetenga asilimia 60 ya bajeti yake katika uwezeshaji ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika.
Katibu Mkuu sekta ya Uchukuzi Bw. Gabriel Migire amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utaibua hoja mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta ya uchukuzi nchini hivyo kuvutia wawekezaji wengi kupitisha mizigo yao Tanzania na hivyo kukuza uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa