Na. Cosmas Njingo (AFISA HABARI)
Serikali imesema itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya Maji, Afya, Elimu, barabara na Umeme, ili kuwaondolea kero Wananchi Wilayani Gairo.
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa kauli hiyo Julai 8, 2021 aliposimama kusalimia na kuwashukuru Wananchi wa Mji wa Gairo kwa kuiamini na kuichagua tena Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwan uliofanyiak Oktoba 2020.
“Nimesikia changamoto zenu, Serikali itaendela kutafuta fedha na kuleta kwenye Halmashauri yenu ya Gairo ili tushirikiane kutatua kero zinazo wakabili hususani kuimarisha miundombinu kwenye sekta ya maji, afya pamoja na barabara”.
Alisema swala la changamoto ya upatikanaji wa maji Wilayani Gairo limekuwa jambo linalo muumiza kichwa na kuongeza kuwa kama mama hapendi kuona wanawake wakipata shida kuhangaika kutafuta maji.
Mhe. Rais Samia alifafanua “Mimi ni mama hili nililisema wakati wa kampeni, inanisumbua kuona wanawake wakihangaika kutafuta maji, kwa hiyo tutahangaika tunavyo weza kuhakikisha maji yanapatikana Gairo”.
Akizungumzia kuhusu sekta ya Afya, Mheshimiwa Samia Alisema swala hilo halina mbadala hivyo serikali yake itahakikisha inatenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa Hospitali za Mikoa na Wilaya, Vituo vya Afya na zahanati kote nchini ili kuwawezesha Wananchi kupata huduma za uhakika za Afya.
“Nadhani kwenye baji tuliyo imaliza juzi, Wabunge wamepewa kiasi kikubwa cha fedha kwa nchi nzima kumalizia maboma ya vituo vya afya na zahanati, kwa hiyo tutakwenda kuhakikisha kuwa hizo fedha zinapatikana kwa haraka ili zahanati zetu na maboma yaweze kujengwa”, alibainisha.
Pia Mheshimiwa Rais akagusia kuhusu usambazaji wa umeme vijijini ambapo alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imetenga fedha za kutosha ili kuhakikisha vijiji vyote vinaunganishwa katika mtandao wa umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijni REA kwa lengo la kuwawezesha Wananchi kupata huduma hiyo kwa uhakika.
Akijibu hoja ya Mhe. Mbunge Ahmedi Shabbiby kuhusu ujenzi wa Madaraja mawili Chakwale na Nguyami pamoja na ujenzi wa barabara inayounganisha Gairo na Wilaya ya Kilindi kwa kiwango cha lami Mhe.Mama Samia alisema Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha madaraja hayo mawili yanajengwa haraka na kuahidi kuwa barabra ya Gairo Kilindi itajengwa kwa kiwango cha lami katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao.
“Hili la barabara ya Gairo hadi Kilindi nalo nimelisikia ila kwa sasa Serikali yangu itashughulikia mapema hayo madaraja mawili aliyoyataja Mhe. Shabbiby Mbunge wenu ili kufungua mawasiliano ya barabara kati ya Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga”, alieleza Mhe. Rais.
Awali Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahmed Shabbiby alimweleza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kuwa barabara inayounganisha Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilindo Mkoa jirani wa Tanga bado ipo kwenye iwango cha vumbi na kwamba barabara hiyo ni kubwa hivyo inahiji kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Mhe. Rais nikwambie tu kuwa barabara inayounganisha Wilaya hizi mbili bado ni vumbi kuanzia Gairo hadi kilindi, lakini tatizo kubwa Zaidi ni ukosefu wa Madaraja imara kwenye Bonde la Mto Chakwale na Mto Nguyami, hivyo tunakuomba hili nalo ulitolee tamko ikiwezekana leo hii ili Wana Gairo wasikie kutoka kwako”, Mhe. Shabibby aliomba.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mhe. Samia Suluhu Hassani kusimama na kuzungumza na wananchi wa Gairo ikiwa ni zaidi ya siku 100 tangu aingie madarakani na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano Hayati Dakta John Pombe Makufuli kilichotokea mwezi Machi 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa