Na/ Cosmas Mathias Njingo; GAIRO
Juni 5.2023
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini anayefanya vizuri katika anga za Kimataifa kutoka Mkoa wa Morogoro Twaha Kiduku, ameungana na Viongozi mbalimbali, Watumishi na Wananchi Wilayani Gairo, kuadhimisha SIKU ya MAZINGIRA DUNIANI kwa kushiriki shughuli za usafi wa Mazingira na ugawaji wa Miche ya Miti.
Akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Jabiri Makame, Kiduku amewataka Wakazi wa Gairo kutunza na kuhifadhi mazingira sambamba na kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi ili kuepukana na hali ya jangwa inayoweza kusababisha ukame.
Awali Mhe. Makame aliwaambia Wananchi hao kuhakikisha kila mmoja anakuwa balozi katika shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi kwenye maeneo yao, kupanda miti kwa wingi na kuhakikisha miti yote iliyopandwa inakua vizuri.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bi. Msifwaki Haule, amempongeza Bondia huyo kwa kuonyesha nia thabiti ya kwenda na kuhamasisha Wananchi wa Gairo kushiriki katika shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira pasipo kujali nafasi yake ya kuwa mtu maarufu nchini.
SIKU ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka, lengo ikiwa ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira sambamba na kuhamasisha Wananchi kushiriki kwenye shughuli za usafi, upandaji wa miti na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa