Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imetenga kiasi cha Shilingi 20,800,000 (milioni ishirini na laki nane) kwa ajili ya ununuzi wa Pikipiki 9 zenye thamani ya Shilingi 2,380,000 kila moja, ambazo zitatolewa kwa vijana wa kikundi cha Boda boda Ibuti kilichopo kata ya Chigela.
Pikipiki hizo ni sehemu ya Mkopo wa 10% unaotolea na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ili kuwezesha vikundi vya Wanawake (4%), Vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%) kujikwamu kiuchumi.
Akizungumza na Afisa Habari wa Halmashauri, Julai 27. 2021, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya Jamii Bwana Isaya Mihinzo alisema Idara yake inaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Serikali ya kuhakikisha kila Halmashauri inatenga 10% ya sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kukopesha makundi hayo kwa kuzingatia vigezo muhimu vilivyo wekwa kwenye miongozo.
“Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuu, hivyo wajibu wetu kama Halmashauri ni kuhakikisha vikundi vyote vilivyo kidhi vigezo vinanufaika na fursa hii adhimu ili viweze kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa kutumia rasilimali fedha zinazo wekezwa kwenye vikundi hivyo au vitendea kazi tunavyo vinavyotolewa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii”. Alisema
Mihinzo alibainisha kwamba katika fedha hizo zilizotolewa kwa ajili ya mkopo wa pikipiki 9 kwa vijana hao wa Ibuti ambao idadi yao inafikia vijana 10, Halmashauri inaandaa utaratibu wa kuongeza pikipiki nyingine moja ili ziwe 10 kulingana na idadi ya vijana hao sambamba na kukamilisha deni la shilingi 620,000 pungufu ya fedha iliyotolewa awali kwenye malipo ya shilingi 20,800,000 ambapo ilitakiwa kuwa shilingi milioni 21,420,000.
“Kimsingi tuna deni la shilingi laki sita na elfu ishirini limepungua katika hizo pikipiki 9, hivyo tupo kwenye mchakato wa kuandaa malipo kwa ajili ya deni hilo pamoja na kuongeza pikipiki nyinine moja ili zifikie 10 kila kijana apate, kwani wapo jumla ya vijana 10 katika kundi hilo”. Alifafanua Mkuu huyo wa Idara ya Maendeleo ya Jamii.
Bwana Mihinzo alisema kuwa huo ni mwendelezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kuhakikisha Wanawake, Vijana na Wenye ulemavu wananufaika na fursa za mikopo ya 10% inayotolewa na Serikali ili kusaidia kuboresha maisha ya watu kupitia ajira binafsi.
“Hii ni fursa ya pekee kwa makundi hayo hasa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu, lengo ni kuhakikisha fursa muhimu kama hizi zinawanufaisha walengwa kwa kuzingatia vigezo vyote na mashariti yanayohitajika”, alifafanua Bwana Mihinzo.
Vijana hao wa Boda boda Ibuti wana tarajiwa kukabidhiwa pikipiki hizo mara tu watakapo kamilisha taratibu muhimu ikiwepo kukatia bima sambamba na kukamilisha usajiri namba za biashara kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania.
Kikundi cha Vijana Bodaboda ibuti ni cha pili kwa upande wa vikundi vya vijana vilivyopewa mkopo wa pikipiki kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo kikundi cha kwanza ni Rubeho Trasporters kupewa Mkopo wa pikipiki 10 zenye thamani ya shilingi Milioni 23,500,000 kwa mashariti ya marejesho bila riba.
Hadi sasa jumla ya vikundi 14 ikiwepo wanawake vikundi 9, walemavu vikundi 3 na vijana vikundi 2 vimekwisha kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mia moja kutokana na 10% ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa