Na. Cosmas Mathias Njingo. GAIRO
Agosti 16.2023.Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirkiana na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta imebuni mikakati ya kukabiliana na tatizo la Sumukuvu katika mazao kwa kutoa mafunzo ya utengenezaji wa Vihenge vya chuma kwa ajili uya kuhifadhia mazao pasipo matumizi ya kemikali.
Jumla ya vijana 17 kutoka Wilayani Gairo walishiriki na kuhitmu mafunzo hayo ya mwezi mmoja yaliyoendeshwa na chuo hicho, yakilenga kuondoa changamoto ya kuwepo kwa sumukuvu katika nafaka aina ya mahindi na karaka kutokana na njia mbovu za uhifadhi wa mazao hayo.
Akizungumza mbele Wajumbe wa Kikao cha Kawaida cha Baraza la Waheshimiwa Madiwani, wakati wa kukabidhiwa vifaa na vitendea kazi kwa ajili ya kutengenezea vihenge hivyo vya chuma, Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Wizara ya Kilimo, aliwaeleza Waheshimiwa Madiwani kuwa; vijana waliopata mafunzo hayo wanatoka katika kata mbalimbali za Wilaya ya Gairo.
Alisema lengo la Serikali ni kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya sumukuvu kwa binadamu, kwani endapo itatumika kwa wingi inaweza kusababisha vifo kwa binadamu na mifugo, hivyo Serikali imekuja na mpango huo ili kuwezesha wakulima kuhifadhi mazao yao katika hali salama zaidi.
“Sumukuvu ikitumika kwa kiwango kikubwa, sote tunajua kuwa madhara yake husababisha vifo kwa watumiaji wa mazao yaliyoathiriwa na ukungu aina ya kuvu ambao hubadilika na kuwa sumu, na endapo sumukuvu italiwa kwa kiwango kidogo inasababisha saratani katika mwili wa Binadamu”. Alibainisha Mratibu huyo.
Mratibu huyo kutoka Wizara ya Kilimo akafafanua kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo, Serikali imetoa bure vitendea kazi maalum kwa vijana hao kwa ajili ya kuanza rasmi mradi wa utengenezaji wa vihenga vya chuma.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Rahel Nyangasi; akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Wahe. Madiwani, aliwapongeza na kuwaasa vijana hao 17 kuvitumia kwa manufaa ya umma na kuvitunza kwa uangalifu ili juhudi za serikali za kupambana na tatizo la sumukuvu zisipote bure.
“Niwapongeze Vijana wote 17 waliohitimu mafunzo, pia ninaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mhe. Rais Dakta Samia, kwa kuendelea kuipendelea Gairo kupitia miradi mbalimbali ya uwezeshaji Wananchi kiuchumi. Rai yangu kwenu; vifaa hivi mkavitunze na kuvitumia kwa manufaa mapana ya kukabiliana na changamoto ya Sumukuvu katika Wilaya yetu ili kuwezesha Wakulima kupata vihenge bora vya chuma vya kuhifadhia nafaka”. Mwenyekiti Nyangasi aliwaasa.
Vijana hao walikabidhiwa jumla ya vifaa tisa kila mmoja ikiwepo Mashine ya kuchomelea, mashine ya kutobolea vyuma, msumeno, evider, Kamba ya kupimia (tape measure), try square pamoja na punch, hivi vyote vinamuwezesha fundi kukamilsha kazi ya utengenezaji wa vihenge bila usumbufu wa aina yoyote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa