Na. Cosmas Mathias Njingo; GAIRO
Februari 24.2025
Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ngazi ya jimbo, Wilaya ya Gairo, wamekutana na viongozi wa dini katika kikao maalum kilicholenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mhe. Rais, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani.
Mkutano huo ambao umefanyika katika ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri Februari 21.2025 umelenga kuhakikisha viongozi wa dini ambao ni wadau muhimu katika jamii, wanashirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwahamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uboreshaji wa daftari hilo muhimu kwa hatima ya ushiriki wa kidemokrasia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Afisa Mwandikishaji Msaidizi wa Jimbo Bi. Jane Sanga, amesisitiza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni zoezi la msingi linalowapa wananchi fursa ya kikatiba ya kushiriki katika kuwapata viongozi wa ngazi mbalimbali kwa njia ya kidemokrasia.
“Tunatambua nafasi kubwa na ushawishi wa viongozi wa dini katika jamii. Kupitia mafundisho na mikusanyiko yao ya kila wiki, wanaweza kufikisha ujumbe wa kuhamasisha uandikishaji wa wapiga kura wapya na wale wanaopaswa kusahihisha taarifa zao,” alisema Bi. Sanga.
Kwa upande wao, viongozi hao wa dini walionesha utayari wao kushirikiana na NEC katika kufanikisha zoezi hilo, wakisisitiza kuwa ushiriki wa waumini wao katika uchaguzi unategemea moja kwa moja na uelewa wao wa umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Mwenyekiti wa mwenza wa Jukwaa la Amani dini mbalimbali, Mchungaji Canon Mmbelwa, alisema wanatambua umuhimu wao katika kuhimiza Waumini wa di ni zote kushiriki katika zoezi la kujiandikisha ili kupata sifa za kupiga kura, hivyo watatumia majukwaa ya ibada kutoa elimu hiyo.
“Tutatumia majukwaa yetu ya ibada kuwaelimisha waumini juu ya wajibu wao wa kikatiba na kiraia. Tunatambua kuwa kushiriki uchaguzi ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya nchi.”
Aidha, mkutano huo ulijadili changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika mchakato huo, ikiwemo upotoshaji wa taarifa mitandaoni, mwamko mdogo wa baadhi ya makundi ya jamii, na hitaji la ushirikiano baina ya wadau wote katika kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuanza tarehe 1na kukamilika tarehe 7 Machi 2025 katika vituo 94 vya kata 18 za Halmashuri ya Wilaya ya Gairo, huku Tume ikisisitiza umuhimu wa kila mwananchi mwenye sifa kujitokeza ili aweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa