Na. Cosmas Mathias Njingo. GAIRO DC
Zikiwa zimesalia siku chache Watanzaia kuingia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23. 2022, huku Serikali ikikamilisha maandalizi ya zoezi hilo, Viongozi wa Vyama vya Siasa Wilayani Gairo wamesema wataendelea kuunga mkono juhudi kwa Serikali za kutoa elimu na kuhamasisha Wananchi kushiriki sensa, kwa lengo la kuhakikisha kila Mwananchi anaelewa umuhimu wa sensa ili ahesabiwe pasipo kikwazo chochote sambamba na kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa Sensa.
Wamesema hayo Agosti 13. 2022, wakati wakishiriki kwenye matembezi ya Hamasa kwa Umma kuhusu Sensa ya Watu na Makazi yaliyoambatana na uzinduzi wa Tamasha la Sensa likichagizwa na michuano ya Ligi ya kuwania kombe la Sensa kwa mchezo wa Mpira wa miguu (Gairo Sencer Cup 2022).
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Gairo Bwn. Ernest Boniphace alisema chama chake kipo tayari kushirikiana na uongozi wa Wilaya kutoa elimu wa Wanachama wa chama hizo na kwa wananchi wengine kwa kuwa zoezi la Sensa ni zoezi muhimu kwa mustakabali wa Serikali kupanga mipango bora ya kuwafikiashia Wananchi wake Maendeleo bila kujali itikadi za vyama na kuongeza kuwa Maendeleo hayana Vyama.
“Sensa ya watu na Makazi ni zoezi muhimu sana kwa Taifa letu, kwani inaiwezesha Serikali yetu kujua idadi ya watu, mahali walipo, mahitaji yao, hali zao za ajira na kipato; ili iweze kupanga na kutoa huduma kwa kuzingatia takwimu zitakazo patikana baada ya Sensa. Ndiyo maana chama cha CHADEMA tumeamua kushiriki kwa nguvu zote kwenye tamasha hili ikiwa ni kuonyesha Umma wa Watanzania kuwa Sensa na Maendeleo havina Vyama bali ni fursa ambayo kila Mtanzania anastahili kuipata”. Alifafanua Bwn. Boniphace.
Naya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya, Bwn. Shabani Sajilo amewataka wenyeviti wa Vitongoji vya Mamlaka ya Mji mdogo pamoja na Wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanashirikiana na Watenda wa Kata na Vijiji kutoa elimu na kukamasisha Wananchi washiriki katika zoezi hili pamoja na kuhakikisha kaya zote zinafikiwa na makarani wa Sensa ili kupata takwimu sahihi.
“Mimi wito wangu ni kwenu Wenyeviti wote wa vitongoji vya Mamlaka ya Mji Mdogo na Wenyeviti wa Vijiji, hili ni jambo lenu na niwajibu wenu kam viongozi kuhakikisha kaya zote zinafikiwa na Makarani wa Sensa na kila Mwananchi amehesabiwa. Mkashirikiane na Watendaji wa Kata na Vijiji katika kusimamia zoezi hili liweze kufanikiwa”. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya ya Gairo.
Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Jabiri Omari Makame akawataka Wananchi wa Gairo kujitokeza kuhesabiwa na kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazo saidia kupanga mipango enedelevu kwa kuzingatia mahitaji ya Wananchi wake.
“Kushiriki Sensa ni wajibu wa kila Mwananchi na kila Mtanzania atakaye lala nchini uskiku wa kuamkia tarehe 23 mwezi wa nane 2022. Kila mmoja awetu akitokeze kuhesabiwa na kuhakikisha taarifa zinazokusanywa ma karani wa sensa ni taarifa sahihi”. Alisema Mhe. Makame.
Mkuu huyu wa Wilaya akatumia fursa hiyo kuwaasa Makarani wa Sensa kuwa waaminifu, wakweli na wazelendo, pamoja na kujiepusha na vitendo vitakavyo hatarisha usalama wa taarifa watakazo zikusanya na maisha yao wenyewe huku akitolea mfanya wa Ngoswe aliyejitumbukiza kwenye mapenzi wakati wa sensa na kusahau majukumu yaliyokuwa mbele yake.
“Kuweni waangalifu, waaminifu na wakweli, lakini pia wajibu wenu ni kukusanya taarifa na siyo kwenda kujiingiza katika vitendo ambavyo vitahatarisha usalama wenu na taarifa mntakazo zikusanya. Tukumbuke habari ya Ngoswe kumpenda Mazoea Binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi na kusahau kazi iliyompeleka pale, nina Imani sote tunajua nini kilitokea”. Aliwaasa.
Matembezi hayo ya Hamasa ya Sensa yaliambatana na uzinduzi wa Tamasha la Sensa likichagizwa na burudani kutoka kwa Wasanii wa Gairo All Stars pamoja na michezo mbalimbali ikiwepo kukimbiza Kuku, Kuvuta Kamba na mchezo wa Mpira wa miguu kati ya Timu ya Watanashati na Lushwaji zilizo fungua mashindano ya kuwania Kombe la Sensa (Gairo Censor Cup).
Aidha tamasha hili lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sensa wakiwemo Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya Gairo All Stars, Makarani wa Sensa, Watumishi wa Taasisizi za Umma, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wafanya Biashara, Walimu na Wananchi lengo ikiwa ni kutoa Hamasa ya Sensa ya Watu na Makazi kwa Wananchi na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa