Wilaya ya Gairo imezindua rasmi zoezi la chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 linalo endelea nchi nzima, ambapo wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mji wa Gairo wamejitokeza kwa shauku kubwa kushiriki kuchanjwa.
Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, chanjo ya UVIKO-19 ilizinduliwa Ikulu Jijini Dar es Salaam Julai 28 2021 na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo katika hotuba yake Mhe. Rais aliwambia Watanzania kuwa swala la uchanjwaji ni la hiari hakuna mamlaka yoyote ya Serikali au binafsi itakayo mshurutisha mtu kuchanjwa.
Wakazi wa Mji wa Gairo wamepokea zoezi la chanjo ya UVIKO kwa ari ya kipekee kwa kuonyesha mwamko na hamasa kubwa ya kuhitaji huduma ya chanjo hali ambayo imeelezwa kuwa ufahamu kuhusu chanjo na kinga ya UVIKO imeongezeka kwa wananchi walio wengi.
Akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mheshimiwa Jabiri Omari Makeme, Katibu Tawala a Wilaya ya Gairo Bwana Augustino Chazua aliwataka wananchi kuendelea kupuuza taarifa za upotoshaji zinazo sambazwa na baadhi ya Wananchi kwamba kinga hiyo ya UVIKO-19 ina madhara makubwa kwa binadamu.
“Yapo maneno maneno ya upotoshaji yanasambaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii hukusu kuwepo na madhara kwenye chanjo hizi za JJ, wapuuzeni hao kwani hawaitakii mema nchi yetu wala hawapendi kuona tunavuka salama katika janga hil”. Alisisitiza Chazua.
Bwana Chazua alibainisha kuwa Viongozi wa Wakuu wa Nchi wakiongozwa na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan wamekuwa mstari wa mbele kusisitiza usalama wa chanjo na wamekuwa mfano kwa kuwa wa kwanza kuchoma chanjo hivyo siyo jambo rahisi kukubali kupata chanjo ambazo zinahisiwa kuwa na madhara kwa binadamu.
“Tumeshuhudia wenyewe jinsi Mama yetu kipenzi akichoma chanjo kwa uwazi tena bila chembe ya shaka. Hivi ni kiongozi gani anayeweza kuweka rehani uhai wake kwa kukubali kuchomwa chanjo ambayo inamadhara”. Alihoji katibu Tawala huyo.
Hata hivyo aliwasisitiza Wananchi kuendelea kuchukua tahadhali na kuongeza juhudi ya udhibiti wa kuzuia maambukizi UVIKO, na kuwakumbusha kukaa mbalimbali, Uvaaji wa maski, unawaji wa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutokusalimiana kwa kushikana mikono sambamba na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Serikali imetoa muongozo wa utoaji wa chanjo ya UVIKO ambapo itakuwa ni ya hiari na vipaumbele ni makundi ya watu watumishi wa sekta ya Afya, watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa sugu ya muda mrefu.
Kimkoa, Morogoro ilizindua chanjo ya UVIKO mnamo Agosti 3, 2021, huku Wilaya ya Gairo nayo ikitekeleza agizo hilo kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika chanjo dhidi ya virusi vinavyo sababisha korona Agosti 5.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa