Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Gairo limewafukuza kazi Mratibu wa Elimu Kata na Tatibu Afya, kwa tuhuma za utoro kazini, pamoja na kuwarejesha kazini watumishi wengine watano wa idara ya ujenzi waliokuwa wamesimamishwa kwa tuhuma za matumizi makubwa ya ujenzi katika mradi wa mabwalo mawili ya Wasichana shule ya sekondari Gairo, jambo ambalo ilidaiwa kutoendana na uhalisia wa ubora wa majengo hayo tofauti na thamani ya pesa iliyotumika.
Uamuzi huo umetolewa Juni 10, 2021, na Mhe. Rahel Nyangasi, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri, katika kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani kujadili taarifa za maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu cha Januari hadi Machi 2021, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Awali kabla ya kusoma maamuzi katika Baraza hilo lililohudhuriwa na Wataalam mbalimbali wa Halmashauri wakiwepo wananchi, Baraza lilijigeuza kama Kamati ili liweze kupitia na kujadili mashauri ya kinidhamu dhidi ya watumishi hao na baadaye kurejea katika mfumo wa Baraza na kutaja maazimio ya kamati mbele ya Baraza.
Alisema “Kamati imeridhika kuwa Mwalimu Laurence Mwamondo ambaye alikuwa mratibu wa Elimu kata, pamoja na Ndugu Malowa Malowa kuwa ni watoro kazini kwa muda mrefu, kama vile haitoshi hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kuwapata hewani hivyo kuiwia vigumu kamati iliyoundwa kuwachunguza kuwapata, kwa maana hiyo natangaza kuwa Baraza hili limewaondoa rasmi katika utumishi wa Umma”.
Akitaja uamuzi huo Mhe. Nyangasi amesema Baraza hilo limefikia maamuzi ya kuwaondoa kazini watumishi hao wawili kutoka idara ya Elimu na Idara ya Afya kwa tuhuma za utoro kazini baada ya Mamlaka ya nidhamu kujiridhisha pasipo na shaka kuwa watumishi hao wameshindwa kutii taratibu, kanuni na sharia za kazi na kuamua kuto onekana kazini kwa muda mrefu pasipo taarifa yoyote.
Watumishi wanne wa idara ya ujenzi waliorejeshwa kazini ni pamoja na Bwana Nassoro Kindamba (Fundi Sanifu Mkuu Mwandamizi), Bwana Josephat Lyombo (fundi sanifu), Bwana Majija Izengo (Fundi Sanifu) pamoja na Bwana Boniphace Chama (Mkadiriaji Majengo).
“Watumishi hawa wa idara ya ujenzi kimsingi tuhuma dhidi yao hazina mashiko, walisimamishwa kazi kwa muda mrefu lakini hakuna hatua za kiuchunguzi zilizo fanyika huku wakiendela kula mshahara wa serikali, hivyo Baraza limeamua warejeshwe kazini na waendelee na majukumu yao ya kuwatumikia Wananchi” alifafanua Mhe. Nyangasi.
Kwa upande mwingine Baraza hilo pia limewafutia tuhuma watumishi wengine watatu wa Idara ya Elimu Msingi baada ya Kamati ya uchunguzi iliyopewa majukumu ya kuchunguza tuhuma ya kujihusisha na wizi wa mitihani ya Taifa ya darasa la saba mwaka 2020, kutowakuta na hatia dhidi ya tuhuma hiyo.
“Kwa Mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa sheria za Baraza la Madiwani leo tarehe 10 Juni 2021, natangaza kuwafutia tuhuma ya wizi wa mitihani Afisa Elimu Msingi Wilaya, Ndugu Zakayo Mlenduka, Afisa Elimu taaluma msingi Bi. Digna Matunda na Ndugu Yusuph Mandia, afisa taaluma msingi”, alitangaza.
Maafisa hao kutoka idara ya elimu msingi walikuwa wakikabiliwa na tuhuma ya wizi wa mitihani ya Taifa ya Darasa la saba iliyofanyika mwaka jana 2020, lakini hata hivyo haijathibitika wazi ukweli wa tuhuma hizo hali iliyo sababisha Baraza hilo kuwafutia tuhuma dhidi yao na kuwataka waendelee kuchapa kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa