Na. Cosmas Njingo GAIRO DC
Serikali imejipanga kuhakikisha inaendelea kuimarisha mifumo yake ya ndani ya utendaji kazi ili kuboresha upatikanaji wa hudma sambamba na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa jamii kupitia matumizi ya TEHAMA na kuwezesha mawasiliano ya Kidijiti kati ya Serikali na Wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati wa kikao cha Ufuatiliaji wa Maendeleo ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, Agosti 2, 2022.
“Kwa sasa Dunia inaelekea kwenye mfumo wa kidijitali ambao unasaidia kuboresha mawasiliano na ufikishaji wa huduma kwa haraka kwa Wananchi kutokana na mapinduzi makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Bw. Daudi alisema kuwa katika kufanikisha adhima hiyo ya Tanzania ya Kidijiti Serikali imebuni mifumo mipya mitatu (3) ambayo itatumika kupima utendaji kazi wa watumishi, kusaidia kuboresha utendaji kazi wa Serikali na Taasisi zake pamoja na kuwezesha wananchi kutafuta huduma kupitia mifumo hiyo mahali popote walipo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
“Katika kuhakikisha tunaimarisha utendaji kazi Serikalini hasa kwa Watumishi wa Umma, tumejaribu kubuni mifumo mitatu (3) ambayo itatuwezesha kuboresha upatikanaji wa huduma sambamba na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa jamii kupitia matumizi ya Dijiti na kuwezesha mawasiliano kati ya Serikali na Wananchi”.Alieleza.
Akitaja mifumo hiyo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi alisema ni pamoja na Mfumo unaolenga Upimaji wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information
System-PEPMIS).
Alisema “Mfumo wa PEPMIS unalenga kupima Kidijiti Utendaji kazi wa Watumshi wote wa Umma mahala walipo namna ambavyo wamejipamabanua katika kuwahudumia Wananchi, ambapo Mwajiri atakuwa na uwezo wa kuona kila siku vile watumishi wanatekeleza maelekezo ya Serikali”.
Mfumo mwingine ni wakupima Utendaji kazi Kitaasisi (Public Institutions Performance Information Management System-PIPMIS) ambao unaiwezesha Serikali kutambua ufanisi wa namna Taasisi zake zinavyotenda kazi na kufunya ufuatiliaji wa utekelelezaji wa shughuli za kila siku wa Taasisi za Umma.
“Mifumo hii miwili yaani ule wa kwanza wakupima watumishi PEPMIS na wa pili wa kupima taasisi PIPMIS inawezesha kufanya ufuatiliaji wa kila siku na kupata taarifa za mwezi, miezi mitatu hadi mwaka mzima. Na hii itasaidia Serikali kujua ni Taasisi gani imehudumia vizuri ama Mtumishi yupi wa Umma amaweza kufikia lango alilokuwa amejiwekea”. Alifafanua Bw. Daudi.
Mfumo mwingine ni wa Saraka ya Serikali (Government Directory) unao waunganisha Watumishi wa Umma na Wananchi katika utoaji wa huduma mbalimbali, ambapo Mwananchi nauwezo wa kutafuta huduma kwa njia ya kidijitali na akahudumiwa pale alipo bila kulazimisha kusafiri kwenda kufuata huduma husika.
Kikao hicho cha kutathmini utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijiti kilihudhuriwa na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ambapo mwenyeji wa Mkutano huo muhimu wa mandeleo ya Taifa ni Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuhusisha pia wadau kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakiwemo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Kupitia mradi huo, UCSAF imepanga kuboresha minara 488 yenye kasi ya 2G kwenda kwenye kasi ya 3G na 4G, ikiwa ni pamoja na kujenga minara mipya 763 katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Bi. Justina Mashiba amesema kuwa mradi huo unaifanya Tanzania kupanua wigo wa matumizi ya kidijiti kwa kasi kubwa hadi kufikia maeneo ya vijijini.
Mradi huo unatokana na ufadhili wa Benki ya Dunia kwa kipindi cha miaka mitano, lengo likiwa ni kuwezesha mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa kidijiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa