Na, Cosmas Mathias Njingo
Gairo, Morogoro
Sepetemba 14.2022
Pamoja na Serikali kuendelea na juhudu za kuboresha miundombinu ya elimu na kuweka mazingira rafiki, wezishi ya kuhakikisha watoto wote wanaostahili kwenda shule, wanapata fursa hiyo bila vikwazo, bado baadhi ya wazazi na walezi Wilaya ya Gairo wamekuwa kikwazo na chanzo cha kuzima ndoto za watoto wa kike kunufaika na fursa za upatikanaji wa elimu.
Imeelezwa kuwa watoto wa Kike kuacha shule na kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kabla ya wakati, ndoa na mimba za utotoni, husababishwa na mila kandamizi zinaendekezwa na baadhi ya makabila Wilayani humo, hali ambayo inachochea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono kwa watoto wa kike wanaotoka kwenye makabila hayo.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Nguzo Imara, Bwn. Stiphene Majumba ametoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Wilaya ya Gairo, uliofanyika Septemba 14, 2022, katika ukumbi wa mikutano wa Halmshauri hiyo, ambapo alibainisha changamoto hiyo ipo kwa kiasi kikubwa kwenye kabila na Wakamba na Wakaguru.
“Wanaochangia kwa kiasi kikubwa watoto wa kike kuacha shule na kuingia kwenye mahusiano ni Wazazi, unaanza na nani au unamuona nani ikiwa mzazi mwenyewe anakwambia huyu ni mwanangu akiolewa wewe inakuhusu nini”. Alisema Bw. Majumba.
Akaongeza kwa kuwaomba viongozi wenzake wa mshirika yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kuondoa hali ya ubinafi kwa kuhakikisha wanapeana uzoefu katika kuandika maandiko mbalimbali ya kuomba misaada kutoka kwa wahidani kwa lengo la kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike na kutokomeza kabisa tatizo la ndoa na mimba za utotoni.
Awali akifungua Mkutano huo wa mwaka wa Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabiri Omari Makame alisema badoo kuna safari ndefu ya kutokomeza ukatili wa kijisia na kumkomboa mwanamke dhidi ya vitendo vya unyanyasaji anavyo tendewa katika jamii sambamba na kupinga mimba na ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.
“Bado tunasafari kubwa sana ya kumkomboa mwanamke dhidi ya manyanyaso yanayotokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kupinga mila kandamizi zinazo sababisha ndoa na mimba za utotoni. Hii itafanikiwa endapo wadau wa maendeleo ikiwepo taasisi za kiraia tutaungana kwa pamoja na Serikali katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.
Mhe. Makame akaongeza kuwa Wilaya ya Gairo bado ipo nyuma kwenye suala la elimu na kwamba jamii ya wakazi wa Gairo haijatambua umuhimu wa kusimamia elimu ili kuwawezesha watoto wao kunufaika na fursa ambayo Serikali imetoa kwa watoto wote wa Kitanzania bila kujali hali zao kiuchumi.
“Unakuta Mtoto anajitahidi darasani na anafaulu, lakini mzazi mwenyewe anamwambia mwanaye asifaulu kabisa mtihanim ahakikishe anafeli kwa madai kuwa hayuko tayari kuendelea kumsomesha. Kibaya zaidi hata mtoto akifaulu anamchukua na kwenda naye mbali mashambani kuonyesha kuwa hataki kabisa kumwacha mtoto wake andelee na masomo”. Alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.
Naye Afisa Ufuatiliaji na Tathimini, Kutoka Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro Ambonisye Haule, alibainisha kuwa mila kandamizi zimekuwa zikibagua utoaji wa haki kwa watoto wa kike huku watoto wa kiume wakipewa upendeleo kwenye mgawanyo wa majukumu na ushuriki maamuzi ya umiliki wa rasilimali za familia.
“Mtoto wa kiume halazimishwi kuacha shule, lakini mtoto wa kike analazimishwa kuacha shule na kubebeshwa majukumu ya kifamilia yasiyo lingana na umri wake tofauti na mtoto wa kiume”.
Mkutano huo wa siku moja wa Jukwaa la Asasi za Kiraia (NGOs) ulihuduriwa na Viongozi mbalimbali wa Asasi hizo, Mashirika ya Dini ikiwepo Umoja wa Madhehebui ya Kikristo Tanzania (CCT), lengo ikiwa ni kupitia taarifa za utekelezaji wa shughili mbalimbali zilizotekelezwa na mashirika hayo kwa kipindi cha mwaka 2021, changamoto zilizojitokeza pamoja na kujadili mikakati ya kutatua changamoto hizo ili kusonga mbele.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa