Serikali imepiga marufku walimu wa vijijini kuhamishiwa mjini pasipo kuwepo na mbadala wa kuziba nafasi hiyo, isipokuwa imetoa kibabali kwa walimu wa mjini wanao hitaji kuhamia vijijini watahama bila mashariti yoyote.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mita (OR-TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Tawi la Tume ya Utumishi wa Walimu Jijini Dodoma Septemba 9.2021.
Ummy alisema “Hakuna mashariti wala vikwazo kwa walimu wa mjini watakao hitaji kuhamia shule za vijijini, isipokuwa mashariti yatawahusu walimu wa vijijini wanao hitaji kuhamia mjini wanalazimika kutafuta wa kubadilishana nao kabla ya kuhamishwa ili kuondokana na upungufu wa walimu kwenye maeneo ya vijijni.
Waziri Ummy akatumia fursa hiyo kuiagiza Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC) kusimamia kikamilifu zoezi la uhaishaji wa Walimu na kuonya kuacha mara moja kuhamisha walimu wa shule za pembezoni mwa Halmashauri pasipo kuwepo mbadala wa kuziba nafasi itakayo achwa wazi na Mwalimu aliyehamishwa.
“Nataka nieleweke vizuri, ni marufuku kuhamisha walimu kutoka katika Halmashauri zilizoko pembezoni, hapa namaanisha walimu wa vijijini kuja mjini kabla ya kupeleka waalimu mbadala kwa ahili ya kuziba hiyo nafasi, hii itasaidia kuondokana na upungufu wa walimu,” Alionya Waziri Ummy
Waziri Ummy akaongeza “Tume ya Utumishi wa Walimu ni wajibu wenu kuhakikisha kwamba Mwalimu anayeomba uhamisho kuja mjini awe ameshapata mbadala wa kuziba nasafi hiyo kabla ya kumhamisha mwalimu yoyote hii itasaidia sana kuondokana na changamoto ya uhaba wa watumishi wa kada ya elimu kwenye maeneo yanayotajwa ni ya mazingira magumu hususani vijijini”. Alisisitiza Msheshimiwa Ummy.
Mhe. Ummy akafafanua zaidi kuwa walimu wanaotaka kuhama kutoka mijini kwenda vijijini hao uhamisho ni ruksa na ufanyike haraka pasipo urasimu wa aina yoyote kwa kuwa shule nyingi zilizopo mijini hazina changamoto kubwa ya upungufu wa walimu ikilinganishwa na shule za pembezoni mwa Makao makuu ya Halmashauri.
Akizungumzia kuhusu walimu walio tumikia eneo moja kwa muda mrefu Waziri Ummy alifafanua kuwa ihakikishwe kunakuwepo na walimu mbadala wa kuziba nafasi inayoachwa na mwalimu anayehama
“Uhamisho ni haki ya mtumishi lakini changamoto kubwa wengi wanataka kuhama kutoka Halmashauri za vijijini kwenda mijini, hili haliwezekani, lakini kama amekaa zaidia miaka mitatu na anahitaji kuhama ihakikishwe kunakuwepo na walimu mbadala wa kuziba nafasi inayoachwa na mwalimu anayehama”, alieleza Waziri Ummy.
Waziri Ummy Mwalimu alisema kuwa Serikali imejikita katika kutoa elimu bora kwa jamii kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia na kuongeza kuwa ni wajibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha uwiano wa walimu unafanyika ili kutoa elimu sawa kwa watoto wote wa Kitanzania hasa kwenye maeneo yaliyoko pembezoni mwa Halmashauri.
Aidha ameitaka tume ya Utumishi wa Walimu kufanya tathmini ya kina kwa kuangalia uwiano wa waalimu kwenye shule za Msingi na Sekondari katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lengo likiwa ni kuwa na takwimu sahihi za mahitaji halisi ya walimu na uwiano uliosawa katika Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa