Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Ndugu Asajile Lucas Mwambambale amesema moja ya majukumu yake makubwa ni kuhakikisha anasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vya ndani vya mapato yasiyolindwa ili kufikia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.084 ifikapo Juni 2022.
Asajile ametoa kauli hiyo Agasti 17.2021 katika kikao chake na Wakuu wa Idara na vitengo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri lengo ikiwa ni kuonyesha dira na kuweka mikakati ya kuboresha makusanya ya ndani ya mapato yasiyolindwa, ikiwa ni siku chache baada yakuripoti ofisini kufuatia uteuzi wa Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Alisema swala la kukusanya mapato ni la kila Mkuu wa Idara bila kujali kada yake na kwamba mapato ndiyo kipaumbele cha kwanza katika utekelezaji wamajukumu yake ya kila siku hivyo ni vyema kutembea na wimbo huo siku zote.
“Mapato siyo ya Muweka Hazina peke yake,ni wajibu kufikiri kwa pamoja, kutenda pamoja na kutekeleza pamoja ukusanyaji wa mapato bila kujali kada zetu”, alisisitiza Mwambambale.
Alifafanua kwamba ili kuvuka daraja hilo ni lazima kufanya vizuri zaidi katika eneo la makusanyo kwa kuhakikisha Halmashauri inavunja rekodi ya makusanyo kutoka kwenye milioni mia sita na kufikia bilioni moja ya makusanyo ya vyanzo vyote.
“Hebu tuachane na lugha ya kutamka milioni mia sita kwenye vyanzo vya ndani vya makusanyo ya bila mapato lindwa, tunatakiwa kuwaza mbali zaidi ya hapo ili kuitafuta bilioni 1.084, hili ndio liwe lengo letu kuu kila siku suki na mchana”, alisisitiza Mwambambale.
Alesema kuwa ni wakati wa kubadilika na kuondokana na dhana potofu ya kuwa kufanya kazi kwenye Halmashauri yenye mapato kidogo ni adhabu na badala yake ugumu huo utumike kama fursa ya kuonyesha uwezo na uweledi katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii
Alitanabaisha “Kufanya kazi kwenye Wilaya ngumu ni fursa, huwezi kuonekana mzuri katika utendaji kama hupitii magumu katika kutekeleza majukumu yako".
Kwa mujibu wa Bwana Asajile ni lazima kufanya mapitio ya vyanzo vilivyopo katika bajeti ya 2021/2022 chanzo kwa chanzo kwa kufanya upemuzi yakinifu sambamba na kuweka malengo ya kukusanya kwa kila chanzo.
Akitaja mikakati ya kuongeza mapato Mkurugenzi Mwambambale alibainisha jambo muhimu ni kutambua vyanzo vingine vipya ambavyo havipo kwenye bajeti ya 2021/2022, kwa kujifunza kutoka Halmashauri nyingine na kisha kuviwekea malengo.
"Kwanza tufanye kazi ya kubainisha vyanzo vingine vipya, kasha kila chanzo lazima kikusanywe kikamilifu. Siyo swala la kuridhika kufika lengo katika chanzo hicho, bali kukusanya zaidi ya malengo kulingana na uwezo wa chanzo husika". Alifafanua
Mikakati mingine aliyoitaja ni pamoja
kushirikisha wadau mbalimbali, viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia Taifa, Mkoa na Wilaya, ikiwepo Serikali Kuu, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Waheshimiwa Madiwani, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Gairo, Chama cha Mapinduzi Wilaya, Wafanya biashara na wadau wengine ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kutekeleza zoei hilo.
Aidha Mwambambale alisema zoezi hilo litakuwa ni kampeni ya kudumu kwa kipindi chote cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kwamba ili kufanikisha hilo ni muhimu kuwa na kauli mbiu ya pamoja inayosema
“Ifanye Gairo Halmashauri Kubwa Kimapato"na kusisitiza kuwa kau;I mbiu hiyo iwe na wimbo kuimba na kuitendea kazi kila siku.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ilijiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi milioni 730,000,000 ikiwa ni makadirio ya makusanyo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani yasiyolindwa ambayo hata hivyo imeelezwa kuwa hayatoshelezi kuendesha halmashauri kwani kiasi hicho hakilingani na gharama za uendeshaji wa shughuli za Halmashauri hivyo ipo haja ya kuongeza nguvu kwenye makusanyo ikiwepo Halmashauri kuwekeza kwenya kilimo bishara cha mazao ya kimkakati kama vile katani na korosho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa