Na, Cosmas Mathias Njingo
GAIRO, Morogoro.
Sepetemba 25.2022.
Hali ya ukosefu maji safi na salama katika kata ya Rubeho Wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro, inaelezwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya ndoa, ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono kwa Wanawake, sambamba na ukatili wa kingono.
Imebainika kuwa baadhi ya wanawake wanakumbana na mateso makali kutoka kwa Waume zao pindi wanapochelwa kurudi nyumbani wakitoka kutafuta maji kwa ajili ya matumiz ya famili. Majo ya ukatili wanaokumbana nao wanawake hao ni pamoja na kukaguliwa sehemu zao za siri wakidhaniwa wametoka kwa Wanaume wengine kufanya mapenzi, kisha kuingiliwa kimwili kinguvu na waume zao bila ridha yao wenyewe.
Kwa mujibu wa utafiti mdogo uliofanywa na Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) katika vijiji saba (07) vya kata hiyo, upatikanaji duni wa huduma za maji safi na salama Katani humo umesababisha ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali ambayo inaelezwa kuwanyima Wanawake haki na uhuru wa kushriki katika kufanya maamuzi mbalimbali pamoja na kuwanyima uhuru wa kujieleza.
kwa Wanaume wengine changamoto ya wivu wa kimapenzi na manyanya “Tunaishi kwa mateso na ndoa zetu ziko hatarini kwa sababu ya wivu wa mapenzi na ugomvi hauishi nyumbani,wenzetu wengine wanakaguliwa ukitoka bombani kuchota maji mwanaume anakukagua maana yake anahisi kwamba umetoka kufanya mapenzi na watu wengine,wanawake wengi wanapigwa mara kwa mara”.
Upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi.
Utumiaji wa maji ambayo sio salama na uhaba wa maji huchangia katika kusababisha milipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu.
Japokuwa maji ni muhimu kwa uhai wa viumbe, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hakuna uwiano wa mgawanyo wa maji ulio sawa kati ya sehemu moja na nyingine na katika majira mbalimbali ya mwaka.
Moja kati ya ukatili wa kijinsia wanaokumbana nao wanawake hao wakiwa katika harakati za kutafuta maji nyakati za usiku ni pamoja na kubakwa wanapokuwa njiani kuelekea ama kutoka maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Joyce Mlimbo Mbalai ni mkazi wa Rubeho wilayani Gairo anaeleza kwamba uhaba wa maji umekuwa tishio kwao hali inayosababisha madhara makubwa kwao hasa unyanyasaji wa wanawake, mabomba hayatoshelezi na maji hutolewa kwa mgao ambayo yanafunguliwa usiku inawalazimu kukesha usiku mzima kusubiria maji.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi ambao ni wenyeviti wa vitongoji kwa namna moja aunyingine nao wanashiriki katika unyanyasaji wa wanawake kwa sababu maji yanapoanza kutoka viongozi hao huanza kujaza maji kwenye matenki na pia wanayatumia kuoshea piki piki na magari yao bila kuangalia hitaji la wanawake walioko katika foleni ya kusubiri maji.
“Tunaishi kwa mateso na ndoa zetu ziko hatarini kwa sababu ya wivu wa mapenzi na ugomvi hauishi nyumbani,wenzetu wengine wanakaguliwa ukitoka bombani kuchota maji mwanaume anakukagua maana yake anahisi kwamba umetoka kufanya mapenzi na watu wengine,wanawake wengi wanapigwa mara kwa mara”.
Hata hivyo alisema kuwa licha ya wanawake wa Rubeho kuhangaika na huduma ya maji usiku kucha kutafuta uhakika wa kuhudumia familia zao, bado wanaume wanashindwa kuwasaidia wake zao hasa kusomba maji hayo kuyarudisha nyumbani.
Alisema kwamba inasikitisha wanaume kushindwa kushirikiana na wake zao licha ya mwanamke kujitolea kutafuta maji kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi mwanaume hatoi mchango wowote hata wa kifedha kumpa mtu wa kukusaidia kubeba maji kuyarudisha nyumbani.
Hivyo mwanamke atalazimika kuuza baadhi ya madumu ya maji aliyochota bombani nyakati za usiku ili kupata hela ya kuwapa vibarua wanaomsaidia kusomba maji ambapo usafiri unaotumika ni toroli linalokokotwa kwa ng’ombe. Anasema kuwa anawashukuru Mtandao wa Jinsia Tanzania.
(TGNP), kufika wilayani Gairo Kata ya Rubeho ambapo baada ya kutoa elimu ya uraghibishi wa changamoto zilizopo kwenye jamii huenda masuala ya ukatili wa kijinsia na ukandamizaji yatapungua kwa sababu baadhi ya wanaume wanalazimisha unyumba bila kuangalia wingi wa majukumu aliyofanya mwanamke kwa siku nzima.
Anasema kwamba hata kama amepata kibarua wa kusaidia kubeba maji kutoka bombani kurudisha nyumbani bado mwanamke analazimika kutoa pesa yeye mwenyewe kwa sababu ya mwanamke kuonekana kwamba ndio mwenye shida ya maji kuliko mwanaume.
Katika hatua nyingine alisema kwamba wanapokosa maji ya kwenye mabomba ambayo
jumla yake yapo tisa katika kata ya Rubeho pekee ambayo hayatoshelezi inawalazimu wanawake kuchota maji katika bwawa la kunyweshea ng’ombe ambayo ni ya chumvi na kusababisha mlipuko wa magonjwa kuhara na kipindupindu.
Anasema kuwa hali ngumu ya maisha kwa baadhi ya wanawake wanapokosa pesa ya kukunua maji laini wanatumia maji ya chumvi yanayopatikana katika bwawa la Figela linalotumiwa kunyweshea ngombe, kufyatua tofali na shughuli nyingine za jamii.
“Tunakutana na matukio mbalimbali katika bwawa la Figela mojawapo sisi wanawake tunapigwa na vijana jamii ya wafugaji kwa sababu wanaona kama vile tunavamia wenye mifugo wanakataza tusichote maji kwenye bwawa lao wanataka ngombe wanywe kwanza, ukitaka kunusurika na kipigo inakulazimu kutoka saa kumi usiku, vinginevyo madumu yanapasuliwa”.
Kwa upande wake Celian Godrick mragibishi kutoka kituo cha taarifa na maarifa Rubeho anasema kwamba changamoto ya maji inafifisha maendeleo ya kitaaluma kwa watoto wa kike kwa sababu inapofika zamu ya kuchota maji usiku inawalazimu kuambatana na watoto wao wa kike, ambapo wanaume wanakuwa wamelala wakati huo.
Anatoa wito kwa mamlaka husika ikiwa ni pamoja na serikali ili kutatua changamoto hiyo ya ukosefu wa maji ili wanawake waweze kufikia malengo yao kiuchumi kwa sababu wanatamani kuwa na nafasi mbalimbali lakini majukumu ya familia yanakuwa ni mojawapo ya pingamizi.
Anasema kuwa mabinti wa kike wanapoamshwa usiku kwenda kuchota maji na mama zao, mara kwa mara wameonekana wakisinzia darasani na kushindwa kumsikiliza mwalimu hali inayosababisha kushuka kitaaluma na wengine kupata mimba za mapema kwa sababu ya kukumbana na ukatili wa kingono nyakati za usiku.
Mariam Makula ambaye ni miongoni mwa wananchi katika kata ya Rubeho alisema kuwa kabla ya maji kutoka bombani wanawake hutumia desturi ya kuweka foleni kwa kutumia kitu chochote kama vile jiwe, sufuria, au ndoo na baadae mwenye foleni anaweza kukinga madumu hata 30, hivyo kuna uwezekano mkubwa wanawake wenyewe kwa wenyewe kutoleana lugha za matusi na kudhalilishana inapobainika kwamba mmojawapo anachota madumu mengi kuliko wengine.
Kwa mujibu wa Mariamu mojawapo kati ya mambo hatari yanayowakumba wanawake
nyakati za usiku ni ubakaji wa mtungo ambapo mwanamke hubakwa na wanaume zaidi ya mmoja hii inatumika kama njia ya kumkomoa mwanamke hasa anaposhindwa kukubali mahusiano kwa urahisi nyakati za mchana.
Ukosefu wa maji umekuwa pingamizi katika maendeleo ya wanawake ambapo miongoni mwa wahanga wamo pia wanafunzi wa kike hasa wanaoishi na bibi zao kwa kujihusisha na foleni za kuchota maji ya usiku kwa sababu ya kuonekana ndio tegemezi kwa familia na mwishowe kupata mimba za mapema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Rubeho chenye wakazi wanaokadiriwa kufikia elfu tano Stanley Adam Mgomba amekiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa maji ambayo inasababisha migogoro ya ndoa na madhila mbalimbali kwa wanawake ikiwa ni pamoja na kuibiwa baadhi ya mali zao nyakati za usiku.
Alisema kuwa ukatili anaoushuhudia mara kwa mara katika ofisi yake ni ukatili wa kiuchumi ambao wanafanyiwa wanawake wengi licha ya kuwa washiriki wakubwa katika uchangiaji wa masuala ya kiuchumi.
Naye Mtendaji Mkuu wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijini RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo alisema kuwa wamepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,029 kati ya miradi hiyo 381 itakuwa ni miradi mipya na miradi 648 ni miradi mikubwa mbayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni ili kuhakikisha kiwango cha uapatikanaji wa huduma ya maji kinaongezeka ili kunusuru hali ya wananchi waishio vijijini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa