Na. Cosmas Mathias Njingo, MOROGORO.
Agosti 6.2023
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) amesema mwaka huu Serikali imepanga kuuza nje ya nchi tani 148,000 za asali hivyo amewataka wafugaji wa nyuki kuzalisha asali hiyo wa wingi ili kutimiza lengo hilo.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Agosti 4 mwaka huu alipotembelea banda la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni siku ya nne tangu kufunguliwa kwa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki.
Waziri huyo amesema kwa sasa asali inayouzwa ni 5% tu hivyo Serikali kupitia Wizara hiyo imepanga kuongeza uzalishaji kwa kutoa elimu kwa wafugaji wa nyuki ili waweze kuongeza kiwango cha uzalishaji na kufikia zaidi ya asilimia 50% ya asali inayouzwa nje ya nchi.
“Tunauza asali nje ya nchi 5% mpango wetu wa Wizara ni kuuza tani 148,000 kwa mwaka huu, maana yake ni kwamba tuzalishe tani 148,000 tuongeze uzalishaji kutoka 5% ikibidi tufike hadi 50%” alsema Waziri Mchengerwa.
Aidha, Mchengerwa ameitaka benki ya Azania ambayo inatoa mikopo yenye riba nafuu ya 1% kwa Wanawake kutanua wigo wa utoaji wa huduma katika maeneo ambayo hayana matawi ya benki hiyo ili kila Mwanamke apate fursa ya kunufaika na huduma za mikopo hiyo.
Akitoa shukrani kwa Waziri huyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameahidi kuandaa mazingira mazuri ya kuhifadhia wanyama ambao wamekuwa sehem ya kivutio kikubwa cha maonesho hayo.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amesema wataweka utaratibu ili maonesho hayo yasiishie kipindi cha Nanenane pekee utaratibu huo utawezesha maeneo hayo kuendelea kuwa kuvutio.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema Kanda ya Mashariki inatafsiri kwa vitendo maelekezo na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake muwakilishi wa Meneja Benki ya Azania Mkoani Morogoro Bw. Josephat Mruma amesema benki hiyo kwa sasa inatoa mikopo ya 1% kwa wanawake ili waweze kujikita katika uzalishaji na kujikwamua kichumi.
Waziri Mchengerwa ametembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika viwanja hivyo na kujionea teknolojia mbalimbali ikiwa leo ni siku ya nne tangu kufunguliwa kwa maonesho hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa