Cosmas Mathias Njingo
Dar es salaam.
Disemba 17.2022
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (MB), amewataka wanahabari kufuata miiko na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kutoa habari na makala zinazochochea amani, mshikamano na furaha ili kuharakisha harakati za kutafuta maendeleo katika jamii, badala ya kuandika habari zinazoweza kuzua taharuki na kuleta machafuko.
Ametoa Rai hiyo wakati wa Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari Nchini lililofanyika Desemba 17, 2022 jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha Wadau mbalimbali wa sekta ya Habari wakiwepo Maafisa Habari Serikalini, Wahariri wa Vyombo vya Habari na waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa Nchini.
“Tumieni kalamu zenu vizuri katika kuhakikisha mnaandika habari na Makala zenye mtazamo chanya unaochochea Amani, Mshikamano, upendo na Umoja, ili kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo katika jamii”. Alisistiza Mhe. Nnauye.
Waziri Nnauye, alisema tasnia ya habari ina wajibu mkubwa wa kulinda maadili, tamaduni na rasilimali za nchi ili kuimarisha tunu zilizo achwa na Viongozi waanzilishi wa Nchi hii kwa kuwa chanzo cha maendeleo katika nchi yoyote ile, ni uwepo wa amani ya kutosha miongoni mwa Wananchi wake.
“Uhuru wa habari ni msingi wa furaha, amani na maendeleo katika jamii na unalindwa kwa mujibu wa sheria na sio utashi wa viongozi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele katika kulinda tunu hii”. Alieleza Waziri Nape
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia ina dhamira ya dhati ya kulinda uhuru wa habari nchini ili kujenga na kuimarisha mahusiano ndani na nje ya Nchi na kwamba Serikali imefanyia kazi mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya huduma za habari na ifikapo Januari 2023 yatawasilishwa Bungeni”, amezungumza Waziri Nape.
Aidha Waziri Nape ameipongeza sekta ya habari nchini kwa kushiriki kikamilifu na kuhakikisha Wananchi wanapata taarifa na elimu ya kutosha kuhusu matukio ya kitaifa na shughuli za maendeleo akitolea mfano janga la uviko 19 na zoezi la Sensa ya watu na Makazi.
“Niwapongeze Wanahabri wote, mnafanya kazi kubwa sana na yaheshima kwa Taifa letu. Niwahakikishie kuwa Wizara ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na wanahabari pamoja na wadau wengine kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi ya kiutendaji, kulinda maslahi ya vyombo vya habari na wanahabari pamoja na kutatua changamoto za sekta ya habari nchini”, amesisitiza Waziri Nape
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema Wizara inatambua mahitaji na haki ya Wananchi kupata habari na huduma za mawasiliano hasa katika wakati huu ambao mabadiliko ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano yamebadilisha mfumo mzima wa utoaji na upokeaji wa taarifa.
Ameongeza kuwa, kupitia Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari ambalo litakuwa endelevu litatumika kama jukwaa la kuwaunganisha Wadau wote wa Sekta ya Habari nchini ili kujadili namna bora ya kuimarisha na kuboresha Sekta ya Habari sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa Vyombo vya Habari Nchini, Bw. Deodatus Balile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeleta mabadiliko mengi katika Sekta ya Habari Nchini, ikiwa ni pamoja na kufungulia magazeti yaliyofungiwa.
Mwakilishi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Michel Toto amesema UNESCO ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali, Asasi za kiraia na wadau wa sekta ya habari nchini ili kukuza sekta ya habari kwa kushiriki kulinda maslahi ya wanahabari; kujenga uwezo na tafiti; utungaji wa sera; kuhamasisha usawa, demokrasia na haki za binadamu katika kukuza maendeleo.
Awali Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Bw Gerson Msigwa alisema Kongamano hilo la kujadili Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini limewakutanisha wadau takribani 1000 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuwakutanisha wadau na kujadili maendeleo ya Sekta kwa ujumla.
“Kongamano hili ni la kwanza kufanyika, lengo kubwa nikuwakutanisha Wadau wa Sekta ya Habari Nchini ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkta Samia aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, yaliyofanyika Mei 3, mwaka huu Jijini Arusha”, amesema Bw. Gerson Msigwa,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa