Na. Cosmas Mathias Njingo.
GAIRO, Morogoro.
Oktoba 21
Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia programu ya kuondoa umaskini kwa Wananchi hususani Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeleta mapinduzi makubwa kwa Vikundi mbalimbali vya Wanawake Wanufaika wa TASAF Wilayani Gairo.
Kikundi cha Neema cha Wanawake, ni mojawapo ya Vikundi vilivyopiga hatua kubwa kiuchumi na kuleta mabadiliko ya kipato cha mwanakikundi mmoja mmoja baada ya kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi zinazowasaidia wana kikundi hao kujikwamua na kupunguza hali ya umaskini miongoni mwao.
Kikundi cha Wanawake Wanufaika wa TASAF cha NEEMA, kilichopo Kitongoji cha Mamuli Kata ya Gairo, wakionyesha bidhaa za Sabuni za Miche na Sukari wanazokopesha kwa lengo la kukuza mtaji wa kikundi hicho. Bidhaa hizo huzitumia wenyewe ama kuuza na kufanya marejesh (Picha na; COSMAS M. NJINGO)
Kikundi hicho kilianzishwa mwezi Machi. 2022, kikiwa na jumla ya Wanachama 15 wote wanawake, kwa lengo la kutafuta fursa mbalimba za kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na umaskini uliokithiri, ambapo kinatekeleza majukumu yake kitongoji cha Mamuli kata ya Gairo.
Baadhi ya Wanakikundi cha Wanawake Wanufaika wa TASAF, katika kikao cha kujadili mapato na maendeleo ya chama pamoja na kukopeshana bidhaa (Picha Na, Cosmas Njingo-GAIRO)
Wanakikundi hao wanasimulia kuwa walianza na mtaji mdogo wa Shilingi 63,000 kwa kununua boksi 2 za sabuni za miche, kila moja ikiwa na sabuni 25, ambazo walikopeshana na wao kwa wao, kwa makubaliano ya kurejesha kiasi cha shilingi 2,500 kwa kila mche mmoja wa sabuni ndani ya mwezi mmoja ili pesa inayopatikana iendelee kuzunguka.
Wanasema baada ya mzunguko wa pesa kuwa mkubwa, kutokana na zoezi la kukopeshana miche ya sabuni, wakaamua kuongeza bidhaa nyingine kwa lengo la kukukuza mtaji pamoja na kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanufaika wa TASAF cha NEEMA, Bi. Mahila Mkunda, anaeleza kuwa, mfumo wa kukopeshana sabuni za miche, umewezesha kikundi hicho kununua mfuko wa sukari wenye ujazo wa Kilo 25, ambazo pia walikopeshana kwa utaratibu wa kurejesha sh.3, 500 kwa kilo.
Baadhi ya masufuria na Viti vya Plastiki vya kikundi cha Wanawake Wanufaika wa TASAF, Neema. Vifaa hivyo vitakodishwa kwenye Sherehe, Misiba na Shughuli mbalimbali za Kiserikali (Picha na Cosmas M. Njingo-GAIRO)
“Baada ya mtaji wetu kuongezeka, tukakubaliana kuongeza bidhaa. Tulimumu Mfuko wa Kilo 25 za sukari ambazo tulikopeshana kila mmoja kilo 3 kwa marejesho y ash. 3,500 kwa kilo. Hii imetusaidia sana kukuza mtaji”. Alisema Bi. Mahila.
Bi. Mahila akaongeza kuwa, kwa sasa mtaji wao umefikia kiasi cha Sh. 1,370,000, ambazo wanapanga kuwekeza kwenye biashara ya kununua alizeti na kuihifadhi kisha kuiuza baada ya bei ya soko kuwa nzuri.
“Mpango wetu ni kununua magunia ya alizeti na kuyahifadhi kwenye ghara kusubiri bei ipande, kisha tutauza kwa bei ya soko kwa wakati ahuo mbapo bei ya zao la alizeti itakuwa imepanda”. Alifafanua Mwenyekiti huyo wa Kikundi cha Neema, kilichiopo kitongoji cha Mamuli.
Naye Katibu wa kikundi hicho Bi. Monica Philipo Malale, alisema, Kikundi na Neema kinatarajia kuanza kutoa huduma ya kukodisha viti, Matenti na masufuria kwenye matukio mbalimbali ya kiserikali na kijamii ikiwepo misiba na sherehe.
“Kiukweli tupo vizuri sana sisi wanawake wa Kikundi cha Neema-mamuli, yaani hivi tunavyozungumza tayari tuna viti vya plastiki zaidi ya 50, masufuria makubwa ya ujazo wa kilo 20 pamoja na bomba za matenti 3 zipo kwa fundi, tunaona kuna fursa kubwa sana ya kwenye sherehe na misiba”, Alisema Bi. Monica.
wamepanga kuanzisha biashara ya kukodisha viti, masufuria na matenti katika shughuli mbalimbali za kiserikali na kijamii kwani tayari baadhi ya vifaa muhimu vimeshapatikana.
Wakitoa maoni yao Wanawake hao Wanufaika wa TASAF kupitia kikundi cha Neema, wamiomba serikali kuwezesha vikundi vya Wanawake Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini, kupata mitaji ya masharti nafuu ili viweze kujikwamua kiuchumi na kusaidia kukabiliana na gharama za maisha.
Vitabu vya kumbukumbu za michango ya Wanachama wa Kikundi cha NEEMA (Picha Na. COSMAS M. NJINGO-GAIRO)
Figure 1Mwenyekiti wa Kikundi cha Neema Bi. Mahila Mkunda akitoa maelezo ya fedha za marejesho ya Wanakikundi hicho kwenye kikao cha Mapato na Matumizi ya Kikundi (Picha Na. COSMAS M. NJINGO-GAIRO)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo-Mtaa wa Malimbika, Kata ya Gairo.
Sanduku la Posta: 40, GAIRO
Simu ya Mezani: +255 787730665
Simu ya Kiganjani: +255 717222572
Barua pepe: ded@gairodc.go.tz, info@gairodc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Haki Zote Zimehifadhiwa